Thursday, August 4, 2016

Mtoto Afia kisimani


DAR ES SALAAM: Majonzi yametanda kwa familia ya  mtoto Gerald (2) ambaye amekutwa amekufa katika shimo la choo cha kanisa linalomilikiwa na mwimba Injili, Boniface Mwaitege, Kipunguni, Ukonga jijini hapa.
Kwa mujibu wa mashuhuda, tukio hilo lilijiri Julai 24, mwaka huu katika kanisa hilo ambalo linakua kwa kasi ambapo awali, mtoto huyo alifika kanisani hapo akiongozana na  mama yake.
Inasemekana kuwa baada ya kufika, mama yake aliingia kanisani kwa ajili ya ibada na kumwacha mtoto wake huyo nje ya kanisa akicheza  na  wenzake.
“Mara baada ya kumaliza ibada jioni, mama huyo alipotoka nje hakumuona mwanaye lakini hakushtuka akijua kuwa  alirudi nyumbani. Alipofika nyumbani hakumkuta, ndipo juhudi za kumtafuta zikaanzia hapo,” alisema shuhuda mmoja.
Akaongeza: “Baada ya juhudi za kumtafuta mtoto huyo kushindikana ndipo wazazi wakatoa ripoti polisi huku waumini wa kanisa hilo wakiendelea na maombi ili mtoto huyo apatikane.
“Siku ya tatu ya kumtafuta mtoto huyo kwa maombi mazito, mwili wake ulipatikana katika shimo la choo cha kanisa ambacho hakijaanza kutumika. Kusema kweli maombi ya waumini naamini yalisaidia na Mungu alituonesha alivyo mwema kwa wanaomwomba.”
Uwazi lilipomtafuta Mwaitege kuhusu tukio hilo, alisema: “Ni kweli tukio hilo lilitokea lakini Mungu ni mwema, mwili wa mtoto ulipatikana na ulipelekwa Morogoro.”
Mwili wa mtoto huyo ulisafirishwa Julai 27, mwaka huu kwenda Ifakara, Morogoro kwa mazishi. Mungu ailaze pema peponi, roho yake. Amina.
 Chanzo: Uwazi