Friday, August 5, 2016

Masikini! Auawa kwa wizi wa nyanya


 

Musoma. Watu wawili, wakazi wa Wilaya ya Musoma Vijijini na Tarime mkoani Mara, wameuawa kwa tuhuma za wizi na ujambazi.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani humo, Erinest Kimola amewataja waliouawa kuwa ni Nyagoma Mase (34), wa Kijiji cha Mayani, Musoma Vijijini na Sererya Moses (20) wa Kijiji cha Masanga Tarime.

Kimola amesema Moses aliuawa Alhamisi saa mbili asubuhi katika Kijiji cha Kukikukwe baada ya kukutwa na debe la nyanya zilizodaiwa kuwa ni wizi mali ya Ibaba Tunga.

Amesema Tunga alipomkuta mtuhumiwa huyo akiwa na debe la nyanya hizo zilizoibwa shambani kwake, alipiga yowe kuita watu.

Amesema watu walikusanyika na kumshambulia kwa kutumia silaha za jadi kisha kuchoma moto mwili wake na kuteketeza nyumba yake ya nyasi na kwamba, tayari watu watatu wamedakwa kutokana na mauaji hayo.