Friday, August 5, 2016

Tundu Lissu Akamatwa na Polisi… Msigwa Ahutubia Iringa

Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amekamatwa na polisi muda mfupi baada ya kuhutubia mkutano wa hadhara katika mji mdogo wa Ikungi, Singida.
Wakati Lissu akiwa mikononi mwa polisi, Mbunge wa Iringa Mjini Mchungaji Peter Msigwa jana alifanya mkutano wa hadhara na kusema hakuna wa kumpangia cha kuzungumza kwenye mikutano yake.
Kukamatwa kwa Lissu 
Lissu, ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Chadema ndiye aliyetoa taarifa za kukamatwa kwake kwenye mtandao akisema: “Wakubwa sana salaam. Ninawaandikieni maneno haya nikiwa chini ya ulinzi wa polisi Singida.
” Nimemaliza kuhutubia mkutano wa hadhara mji mdogo wa Ikungi ambao ni makao makuu ya Jimbo langu la Singida Mashariki. Mara baada ya kushuka jukwaani nimefuatwa Regional Crimes Officer (RCO) wa Mkoa wa Singida aliyejitambulisha kwa jina la Babu Mollel na kunitaarifu kuwa ameelekezwa na Regional Police Commander (RPC) Singida nikamatwe apparently (dhahiri) kuna amri ya kunikamata iliyotoka Dar es Salaam.
 “Kwa hiyo niko nguvuni na ninasubiri maelekezo ya RPC juu ya wanakotakiwa kunipeleka. It’s likely (inawezekana) nitasafirishwa Dar usiku huu. In fact (hakika) ni usiku huu kwa taarifa za sasa hivi. Kwa vyovyote itakavyokuwa, there’s no turning back. There’s no shutting up (hakuna kurudi nyuma, hakuna kunyamaza).
“Nitapambana kutetea haki yetu ya kuwasema watawala popote nitakapokuwa, whether in freedom or in jail (niwe huru au jela)… Aluta continua!. “
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Thobias Sedoyeka  alithibitisha kukamatwa kwa Lissu lakini alikataa kutoa sababu za hatua hiyo.
Chadema jana jioni ilitoa taarifa kuhusiana na kukamatwa kwa Lissu ikisema: “Tunaweza kuthibitisha kwa vyombo vya habari kuwa Mwanasheria Mkuu wa Chama Mh. Tundu Lissu anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Singida kwa sababu ambazo hazijawekwa wazi.” 
Taarifa hiyo iliyotolewa na Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene ilibainisha kuwa Polisi walimkamata jana jioni baada ya kumaliza mkutano wake wa hadhara alioufanya Ikungi jimboni kwake na kueleza kuwa viongozi wa chama hicho mkoani humo walikuwa polisi kuhakikisha anapata haki zake kama inavyostahili na kwamba ofisi ya katibu mkuu inafuatilia kwa ukaribu kujua sababu hasa ya kushikiliwa kwake na kutoa msaada wa haraka kadri itakavyohitajika.
Lissu amekuwa kwenye misukosuko na Jeshi la Polisi mara kadhaa na kwa siku za karibuni alikamatwa na kufikishwa mahakamani akituhumiwa kutoa maneno ya uchochezi kwenye gazeti la Mawio.
Sambamba na kesi hiyo, Lissu alikamatwa na polisi kwa madai ya kutoa maneno ya uchochezi baada ya kupata dhamana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Msimamo wa Msigwa 
Mkoani Iringa, Msigwa akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa kwanza wa kibunge tangu alipochaguliwa uliofanyika kwenye viwanja vya Mwembetogwa mjini hapa, alisema hakuna wa kumpangia hoja za kuzungumza kwenye mikutano yake.
Juzi, mbunge huyo alipewa barua na Jeshi la Polisi iliyoeleza kuwa imempa kibali cha kufanya mikutano hiyo, lakini ikimuwekea masharti mbalimbali likiwamo la kutozungumzia viongozi wengine na badala yake ajikite kwenye shughuli za maendeleo na kuchukua maoni ya wananchi anaowawakilisha.
Pia, alitakiwa kuhakikisha kuwa hakuna mtu kutoka nje ya Mkoa wa Iringa au eneo lolote lililo nje ya mamlaka atakayeruhusiwa kuzungumza.
Lakini jana akihutubia alisema: “Ninaona watu wote mna nyuso za hofu na mimi nimekuja kuwaondoa hofu …hakuna mtu mwenye mamlaka ya kunipangia cha kuzungumza, sipo hapa kwa matakwa ya polisi … mimi nipo kwa matakwa ya kisheria na ninazungumza kwa mamlaka mliyonipatia.
 
 “Pia Katiba inaeleza wazi mad raka na kinga ya Mbunge… mbunge anayo haki ya kuitisha na kufanya mkutano wa hadhara kwa mjibu wa sheria.” 
Kuhusu Rais kuzuia mikutano ya vyama vya siasa, Msigwa alisema hakubaliani na hatua hiyo kwa madai kuwa kufanya hivyo ni ukiukaji wa Katiba ya nchi na Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 ambavyo nchi inayoongozwa chini ya utawala wa kidemokrasia inapaswa kuvifuata.
 “Ninamuunga mkono na ninampongeza Rais John Magufuli kwa kupambana na ufisadi, anapinga rushwa… lakini siungani naye kwa kitendo chake cha kukandamiza demokrasia nchini na niwaombe wananchi wa Iringa kuungana na mimi kumpinga mtu anayekandamiza demokrasia nchini,” alisema.
Kuhusu Serikali kuhamia Dodoma, mbunge huyo ambaye pia ni waziri kivuli wa Wizara ya Mambo ya Nje, alikosoa uamuzi huo akisema hajawahi kuona katika mipango yote iliyowasilishwa na Serikali bungeni inayoelekeza hilo.
“Serikali ilileta mpango wake wa miaka mitano, mwaka mmoja na Bajeti, hivi vyote vinaletwa bungeni na baada ya kujadiliwa na kupitishwa, vinatungiwa sheria ili viweze kutekelezwa hivyo vipaumbele vyake ni lazima vifiti kwenye mipango hiyo,” alisema Msigwa na kuongeza:
 “Lakini katika vyote vitatu vya mwaka huu, mpango wa miaka mitano, mwaka mmoja na hata katika bajeti ya mwaka huu sijaona mahali popote palipoandikwa kipaumbele cha Serikali ni kuhamia Dodoma.” 
Msigwa alisema kuhamisha Serikali ni gharama kubwa na kuwataka wakazi wa Iringa na maeneo mengine kuhoji suala hilo kama ndicho kipaumbele cha maendeleo na mahitaji yao.
Alisema wamejipanga kufanya shughuli za maendeleo ikiwamo miradi ya barabara, kuboresha huduma za afya, usafi wa mazingira na miundombinu.
Mkutano huo ulihudhuriwa na madiwani wa halmashauri hiyo wakiongozwa na Mstahiki Meya, Alex Kimbe.