Sunday, September 4, 2016

Magufuli amaliza ubishi nani Rais halali Zanzibar

ZIARA ya Rais John Magufuli visiwani Pemba imemaliza ubishi wa kisiasa na maneno ya kejeli kutoka kwa wafuasi wa Chama cha Wananchi (Cuf) dhidi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) visiwani humu.
Wanachama hao walilazimika kuondoka katika uwanja wa Gombani ya kale huku wakikata tamaa baada ya Rais kusema kwamba uchaguzi mwingine utafanyika mwaka 2020 na kwamba Rais Ali Mohamed Shein ndiye kiongozi mkuu wa halali wa Zanzibar aliyechaguliwa kikatiba.
Wafuasi wa CCM na Chama cha Wananchi kwa muda wa miezi saba sasa wamekuwa katika malumbano ya kisiasa na mabishano ambapo wa Cuf wamekuwa wakisema kuwa uchaguzi wa marudio wa Machi 20, mwaka huu ulikuwa batili, jambo linalozifanya jumuiya za kimataifa zisiutambue.
Malumbano hayo yalishika kasi zaidi kutokana na ziara za mara kwa mara za Katibu Mkuu wa Cuf, Seif Sharif Hamad nje ya nchi. Seif aligombea urais Oktoba mwaka 2015 na kushindwa.
Ziara hizo zinatajwa kuwapa matumaini wana-Cuf kuwa serikali inayoongozwa na Dk Shein haitadumu.
Baadhi ya wakazi wa Pemba waliupongeza ujio wa Rais Magufuli wakisema kuwa ujio wake umemaliza ubishi uliodumu kwa zaidi ya miezi saba kutoka kwa wafuasi wa Cuf waliokuwa wakisisitiza kuwa Serikali iliyopo madarakani itaondoshwa kwa nguvu za jumuiya za kimataifa.
Mkazi wa Chake Chake, Pemba, Asha Said, alisema amefurahishwa na kauli za Rais Magufuli zenye ukweli na uwazi hasa alipowajibu wapinzani kwamba hakuna uchaguzi mwingine hadi mwaka 2020.
Mabaraza ya Cuf katika jimbo la Chake Chake na Wawi, yalionekana kudorora huku watu wengi zaidi wakiijadili hotuba ya Rais Magufuli aliyoitoa Ijumaa visiwani Pemba.
Mfuasi mmoja wa Cuf katika eneo la Wawi, Pemba aliyejitambulisha wa jina moja la Said, alisema wanamsubiri Katibu Mkuu wa chama chao, Maalim Seif atoe kauli kuhusu hotuba hiyo ya Rais Magufuli.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mberwa Hamad Mberwa, alisema hotuba ya Rais Magufuli ni mwiba mkali kwa wapinzani kwa kuwa imeweka hadharani ukweli wa mambo.
Mberwa aliwataka wanachama na wafuasi wa CCM kusikiliza kauli za Rais Magufuli za kuimarisha umoja na mshikamano kwa kujenga chama ili kuendelea kuwepo madarakani. Alisema ukweli wameufahamu na kuujua na huu si wakati tena wa kupoteza muda na kuingia katika malumbano ya kisiasa kwa viongozi wanaoota ndoto za mchana.