Sunday, September 4, 2016

Bodi ya Mikopo kumwaga fedha kwa waombaji wote

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imesema wale wote walioomba mkopo mwaka huu na kukidhi vigezo watapewa.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru alisema hayo juzi mjini hapa wakati wa hafla ya kukabidhi vyeti kwa watu watano waliorejesha mkopo wa elimu ya juu kwa mkupuo na kwa hiari.
Badru alisema idadi ya walioomba mkopo mwaka huu ni wanafunzi 88,000 ambao bodi itahakikisha wale wote waliokidhi vigezo, wanapatiwa fedha kwa ajili ya elimu ya juu.
Mkurugenzi huyo ambaye amehimiza walionufaika na mikopo kulipa madeni yao, alisema mwaka jana, wanafunzi waliokopeshwa ni 55,000.
Kuhusu waliopewa vyeti ikiwa ni hatua ya kuwatambua, ni pamoja na mfanyakazi wa VETA Shinyanga, Richard Jafu aliyerejesha kwa mkupuo Sh 14,749,950 na Francis Mwilafi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo aliyelipa Sh 15,115,200.
Wengine ni Mbunge wa Vwawa, Japhet Hasunga aliyerejesha Sh 255,000; Profesa Peter Msoffe ambaye ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo cha Dodoma (UDOM) aliyerejesha Sh 1,430,749.
Mwingine ni Mbunge wa Biharamulo, Oscar Mukasa ambaye kiasi alichorejesha hakikutajwa ingawa mkurugenzi mtendaji wa HESLB, alisema amerejesha kiasi kikubwa kwa mkupuo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wadau hao walisisitiza umuhimu wa wanufaika wa mikopo kuirejesha kwa hiari ili kuiwezesha bodi hiyo kukopesha wanafunzi wengine.
Mbunge wa Biharamulo, Mukasa alishauri bodi hiyo kuangalia uwezekano wa kurekebisha vigezo kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi watokao maeneo ya pembezoni kunufaika na mikopo hiyo ya elimu. Kwa upande wake, Mbunge wa Vwawa, Hasunga alisisitiza wabunge wanaodaiwa warejeshe mkopo kwa mkupuo.