Sunday, September 4, 2016

Mhasibu kizimbani kwa kumtusi Rais Magufuli

MHASIBU wa shule ya sekondari ya Mtakatifu Joseph, Elizabeth Asenga (40), amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashitaka ya kumkashifu Rais John Magufuli kwenye mtandao wa WhatsApp.
Elizabeth alifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka na Wakili wa Serikali, Leonard Chalo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.
Wakili Chalo alidai kuwa, Agosti 6, mwaka huu, huku akijua Elizabeth alituma ujumbe wenye mazingira ya kumkashifu Rais Magufuli kwa njia ya WhatsApp kwenye kundi la kijamii liitwalo STJ Staff Social Group. Inadaiwa aliandika ujumbe unaosema:
“Goodmorning humu, hakuna rais kilaza kama huyu wetu duniani, angalia anavyompa Lissu umashuhuri, fala lile, picha yake ukiiweka ofisini ni nuksi tupu, ukiamka asubuhi, ukikutana na picha yake kwanza, siku inakuwa mkosi mwanzo mwisho”.
Baada ya mshitakiwa kusomewa mashitaka, alikana kutenda kosa hilo na upande wa Jamhuri ulidai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba kesi hiyo iahirishwe hadi tarehe nyingine.
Mshitakiwa aliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili, wanaotakiwa kusaini dhamana ya Sh milioni mbili. Kesi itatajwa tena Septemba 22, mwaka huu.
Katika hatua nyingine, mfanyabiashara Juma Shaban (31) amefikishwa mahakamani hapo akikabiliwa na mashitaka sita likiwemo la kutakatisha dola za Marekani 340,000, sawa na Sh milioni 680.
Wakili wa Serikali, Esterzia Wilson, alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Emmilius Mchauru kuwa, Mei 31, 2003, Dar es Salaam, kwa nia ya kudanganya alighushi hati ya forodha akidai anasafirisha madini aina ya dhahabu kwa Igor Davydakin.
Aidha anadaiwa kughushi hati nyingine na stakabadhi kwa nia hiyo, pia alighushi hati ya kusafirisha mizigo akionesha kwamba ndege ya Qatar ilikuwa inasafirisha na kupeleka madini hayo kwa Davydakin.
Esterzia alidai kati ya Aprili 20 na Mei 10, 2013 jijini Dar es Salaam, kwa nia ya kudanganya mshitakiwa huyo alijipatia kiasi hicho cha fedha kutoka kwa Davydakin kwa madai atampelekea madini hayo huku akijua si kweli.
Inadaiwa, mshitakiwa alijihusisha na utakatishaji wa fedha, kwa kuelekeza fedha hizo ziwekwe kwenye akaunti ya Monteblanc Godmine Company iliyopo benki ya Stanbic, na baadaye kuzitoa huku akijua fedha hizo ni mazao ya kosa la kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Mshitakiwa alikana mashitaka na kurudishwa rumande kwa kuwa mashitaka ya utakatishaji fedha hayana dhamana. Kesi itatajwa tena Septemba 15, mwaka huu.