Thursday, December 29, 2016

Francis Cheka atangaza kustaafu ngumi

Bingwa wa dunia wa ngumi za kulipwa mwenye rekodi ya kutopoteza kirahisi mechi zake,kutoka nchini Tanzania anayepigana uzito wa kati Francis Cheka ametangaza rasmi kuachana na mchezo huo wa ngumi na kujielekeza kwenye masuala binafsi ya kibiashara.

Cheka,ngumi jiwe,mwana wa Morogoro amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Morogoro kuhusu taarifa zilizoripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari na kuzagaa kwenye mitandao ya kijamii vikimhusiha na utapeli wa kukimbia ulingoni Dec 25 mwaka huu huko jijini Dar es Salaam, alikotakiwa kupigana na bondia Dula Mbabe,ambapo amebainisha kutofika ulingoni siku hiyo hakukumaanisha kuhofia pambano hilo bali ni kutokana na promota wake Kaike Selagi kutomlipa fedha zake zote kama walivyokubaliana, ambapo amedai alipaswa  kulipwa milioni tisa,lakini hadi wanamaliza kupima uzito alikua amepewa milioni tatu pekee.

Akizungumzia azma ya kuachana na ngumi,Cheka amesema kwa muda mrefu amekuwa akipigana bila mafanikio kutokana na kudhulumiwa na waandaaji au kulipwa tofauti na makubaliano sambamba na misukosuko ya hapa na pale anayofanyiwa na wapinzani wake na kwamba anaamini wapo baadhi ya watu waliolenga kumshusha kwenye ngumi badala ya kumtengeneza bondia mwingine mwenye uwezo na kumpiga na kwamba kwa sasa atajielekeza kufanya biashara zake na kuahidi ushirikiano kwenye mchezo wa ngumi ili kukuza na kuendeleza mchezo huo.

Chanzo: ITV