Wednesday, January 11, 2017

Wanne mbaroni kwa kuua, kumtoa utumbo


Babati. Watu wanne wanashikiliwa kwa tuhuma za mauaji ya Mkazi wa Kijiji cha Lalaji wilayani Hanang’ Mkoa wa Manyara, Ngimba Siima (52).

Siima ameuawa kwa kupigwa na silaha butu kichwani na tumboni kisha kutolewa utumbo.
Kamanda Massawe amesema miongoni mwa watuhumiwa hao wanaodaiwa kufanya mauaji hayo yumo mke mdogo wa marehemu, mdogo wake na watu wengine wawili.

Amesema chanzo cha mauaji hayo inadaiwa ni kutaka kugawana mali za Siima, ikiwamo nyumba, ng’ombe,mashamba na vitu vingine alivyokuwa anamiliki.

Kamanda Massawe amesema inadaiwa kuwa kuna mtu alilipwa Sh500,000 kwa ajili ya kufanya mauaji hayo.

Chanzo: Mwananchi


Katika hatua nyingine, watu watatu wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kukutwa na kilo 38.5 za nyama ya nyati bila ya kuwa na kibali.
Kamanda Massawe amesema kuwa watuhumiwa hao walikamatwa wakati wakiwa wamebeba nyama hiyo kwenye pikipiki katika eneo la Mlima wa Simu Kata ya Njoro lililopo wilayani Kiteto.
“Watu hao walikamatwa wakiwa kwenye pikipiki tatu tofauti walizokuwa wanazitumia kubebea nyara hizo za Serikali. Hadi sasa tunawashikilia wao, nyama na pikipiki walizokuwa nazo,” amesema Massawe.