Sunday, May 28, 2017

Baba wa kambo adaiwa kumnyonga hadi kufa mtoto wa mkewe

MTOTO Agatha Raphael (2), aliyepotea katika mazingira ya kutatanisha, katika kijiji cha Mao, wilayani Kalambo, mkoani Rukwa, amekutwa amekufa kwa kunyongwa na mwili wake kutupwa shambani
Tukio la kunyongwa kwa mtoto huyo, linadaiwa kufanywa na baba yake wa kambo, Mei 16, saa 11:00 jioni.
Taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando, ilisema kabla ya mtoto huyo kuuawa kwa kunyongwa, alipotea katika mazingira ya kutatanisha akiwa na baba yake wa kambo.
Alisema, siku ya tukio, mama mzazi wa mtoto huyo, Anisia Kasiti (22), alikwenda mashine na kumuacha mwanaye nyumbani.
Kamanda Kyando alisema, siku kadhaa kabla mtuhumiwa kufanya mauaji hayo, alisikika akiongea kuwa lazima amuue mtoto huyo kwa kuwa si wa kwake.
Alisema baada ya kauli hiyo, mtoto Agatha alitoweka katika mazingira ya kutatanisha na Mei 17, mama wa mtoto huyo alienda kutoa taarifa kwa uongozi wa kijiji na juhudi za kumtafuta zilianza bila mafanikio.
Mei 18, mama wa marehemu alienda kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi Matai na jalada la uchunguzi lilifunguliwa.
Alisema mtuhumiwa alishikiliwa na polisi kwa uchunguzi kufuatia kauli aliyoitoa, huku juhudi za kumtafuta mtoto zikiendelea.
Kamanda Kyando, alisema Mei 24, majira ya 11:50 jioni, mkazi wa kijiji hicho, Aron Mwanambogo, aligundua kuwapo kwa mwili wa marehemu Agatha shambani kwa mtuhumiwa, ukiwa umelala chali kwenye kijito kilichopo ndani ya shamba hilo.
Alisema baada ya uchunguzi wa kitabibu, iligundulika kuwa mtoto huyo alikufa kutokana na kukosa hewa baada ya kunyongwa .
Mtuhumiwa anaendelea kushikiliwa na polisi na anatarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya upelelezi wa awali kukamilika.
Kamanda Kyando, aliwataka wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mikononi kwa kutoa taarifa kwenye vituo husika iwapo itatokea matatizo ya kifamilia na ndoa.


    TANGAZO