Tuesday, May 30, 2017

Waliotumbuliwa wanalipwa Sh480 milioni kwa mwezi

Dodoma. Maoni ya upinzani ya wizara mbili, jana yaliibua hoja tofauti; ya kwanza ikidai Serikali inawalipa wakurugenzi 120 waliotumbuliwa Sh480 milioni, na ya pili ikikikishutumu kiti cha Spika kwa kuzuia mjadala wa wabunge kutishiwa maisha.
Katika sakata la kwanza, wapinzani walisema fedha za Serikali zinapotea kutokana na watumishi waliotumbuliwa au kuachwa katika uteuzi kuendelea kulipwa stahiki zao.
Msemaji wa kambi hiyo, Japhary Michael alisema wakati akitoa maoni kuhusu bajeti ya Tamisemi kuwa wakurugenzi hao wanalipwa mshahara wa Sh5.76 milioni kila mmoja kwa mwezi.
“Ikumbukwe kuwa wakurugenzi hawa bado wanalipwa mishahara yao pamoja na stahiki nyingine za kiutumishi kama nyumba, umeme, simu, matibabu na kadhalika. Wastani wa mshahara wa mkurugenzi ni Sh 3.8 milioni mpaka Sh4 milioni,” alisema.
Alisema wakurugenzi 120 wa zamani hawakuteuliwa kwa nafasi hizo katika Serikali ya Awamu ya Tano lakini bado wamo katika utumishi wa umma, na hata wale wapya walioteuliwa walitoka nje ya mfumo wa utumishi wa umma, wengi wao wakiwa makada wa CCM.
Alisema baada ya kutenguliwa kwa wakurugenzi hao 120 kutoka halmashauri mbalimbali nchini, walielekezwa kuripoti kwa makatibu tawala wa mikoa waliyotoka kwa ajili ya kupangiwa kazi nyingine.
“Ni zaidi ya mwaka mmoja sasa wakurugenzi hawa takribani wote wanahudhuria kwa makatibu tawala wa mikoa na kimsingi hawana kazi za kufanya,” alisema.
Alisema kambi hiyo inaishauri Serikali kuangalia upya sheria ya utumishi na ajira katika serikali za mitaa ili kuwe na utaratibu ambao mchakato wake utaanzia katika vikao kisheria vya halmashauri.
Michael, ambaye ni mbunge wa Moshi Mjini (Chadema), alishauri Waziri ateue kutokana na orodha itakayopendekezwa na halmashauri baada ya watu kuomba ajira.
Katika sakata la pili, msemaji wa kambi ya upinzani bungeni anayehusika na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ruth Mollel alidai kiti cha Spika kilizuia mjadala wa wabunge kutishiwa maisha kwa mgongo wa kanuni za Bunge.
Suala hilo lilimfanya waziri husika, Jenista Mhagama kusimama na kutaka sentensi hiyo ifutwe kwa kuwa ilishaondolewa wakati kiongozi wa upinzani bungeni, Freeman Mbowe alipokuwa akisoma maoni yao kuhusu bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Lakini hoja hiyo ilipingwa na mbunge wa Iringa, Mchungaji Peter Msigwa aliyesema kuwa Katiba inawapa uhuru wa kusema maneno hayo.
Hata hivyo, Spika Job Ndugai alisema maoni hayo yaliandikwa na mtu ambaye haelewi taratibu za Bunge na hivyo kufuta sentensi hiyo.
Alihoji kama kuna mbunge aliyepeleka taarifa ya kutishiwa maisha.
Kuhusu hoja kwamba wapinzani wanadhibitiwa, Ndugai alihoji wanadhibitiwaje.
“Hivi kwa nini mnajiweka katika hali fulani ya kuona kwamba mnaonewa? Hivi unaonewa na nani kanuni ni za wote? Taratibu ni za wote hakuna mtu aliyedhibitiwa chochote,” alisema.
Chanzo: Mwananchi Communication.