Tuesday, May 30, 2017

Maajabu ya pacha walioungana, wajikuta katika penzi moja

Si rahisi kufikiria maisha ya ndoa ya Maria na Consolata kwa jinsi walivyo, lakini pacha hawa walioungana wako wazi kuhusu matamanio yao ya maisha ya ndoa.
Katika mazungumzo yao na gazeti hili, Maria na Consolata waliweka bayana mipango yao ya ndoa mara watakapomaliza elimu ya chuo kikuu.
Ingawa ni kitu cha kushangaza, Maria na Consolata hawatakuwa mapacha wa kwanza katika maisha ya ndoa. Chang na Eng Bunker ni pacha wanaume waliozaliwa mwaka 1811 nchini Thailand ambako zamani kuliitwa Siame.
Tofauti na mapenzi ya akina Maria na Consolata, pacha hao kila mmoja alioa mke wake na kufanikiwa kupata watoto.
Kama ilivyokuwa kwa pacha hao, Maria na Consolata wanatamani kuwa wanandoa na ndoto zao ni kuolewa na mwanaume mcha Mungu na atakayewajali.
“Ndoa ni sakramenti takatifu, tukishamaliza masomo yetu ya chuo kikuu tunatamani kuja kuwa wanandoa,” anasema Maria.
Kwa namna walivyo, si rahisi kwao kuolewa na wanaume tofauti isipokuwa mume mmoja na wanalijua hilo.
Haya ndio yalikuwa mahojiano baina yangu na wao kufuatia ndoto hiyo.
Mwandishi: Baada ya masomo, nini ndoto zenu?
Maria: Ndoto zetu ni kuwa wanandoa. Zamani tulikuwa tunapenda tofauti, lakini kwa sasa tumempenda mtu mmoja. Tumegundua tuna hisia moja.
Mwandishi: Tayari kuna mtu mmempenda nini?
Maria na Consolata kwa pamoja: Ndio tumempenda mtu mmoja.
Mwandishi: Nani alimwambia mwenzake kwanza kuhusu hisia za kupenda?
Consolata: Sisi ndio tuliomwambia kwamba tunampenda, naye alitusikiliza.
Mwandishi: Aliwajibu nini?
Maria: Yupo kwenye tafakari, hawezi kusema akurupuke na kuingia bila tafakari. Lazima tumpe muda wa kutafakari.
Mwandishi: Ni mwanaume wa aina gani mnayempenda?
Consolata; Tunapenda kuolewa na mwanaume wa kawaida, mwenye tabia njema na mcha Mungu asiwe tajiri. Ikiwa tutamaliza masomo yetu, huyu tuliyempenda anafaa kuwa mume wetu.
Kihalisia tunatamani mwanaume mcha Mungu, mwenye upendo na ambaye atathamini utu wetu.
Mwandishi: Kwa nini hampendi kuolewa na tajiri?
Consolata: Ni kwa sababu matajiri wengi huwa wanathamini pesa zao sio utu. Samahani hapa sio matajiri wote, ila wengi wao kwa hiyo sisi tunataka mtu anayeweza kuthamini utu.
Mwananchi: Ndoa ni mume na mke mmoja kwa Wakristo. Mmewahi kutafakari hilo?
Consolata; Ndio, Biblia inasema kwamba Mungu aliweka agano kati ya mume na mke mmoja. Sasa kwa kuwa sisi tumeungana wawili na tuna hisia moja, hatuwezi kuolewa na wanaume tofauti. Tutaolewa na mume mmoja.
Tunatamani sana kumtumikia Mungu kupitia sakramenti ya ndoa. Mungu akitujalia tumalize masomo yetu basi tunataka kuolewa ili tumtumikie Mungu katika huo wito vizuri.
Pacha hao waliweka bayana jina la kijana waliyempenda, ingawa kwa sababu za kimaadili tunalihifadhi. Hata hivyo, baba mdogo wa kijana huyo alikuwa tayari kuzungumza na gazeti hili.
Baba huyo mdogo alisema ana taarifa za kijana wao kupendwa na pacha hao.
“Unajua nilishangaa kuona watu wananiita baba mkwe wa akina Maria na Consolata. Baadaye ndio nikajua kuwa kuna mahusiano baina yao (kijana na mapacha hao), japo wote wanaendelea na masomo. Kupenda ni moyo na kama ikitokea wakafikia ndoto hizo huko baadaye, basi itakuwa hivyo,” anasema.
Mwalimu mkuu wa Shule ya Maria Consolata, Jefred Kipingi anasema hisia za kuolewa kwa mabinti hao ni jambo la kawaida na kwamba, wanapenda kuishi maisha ya kawaida kama walivyo watu wengine.
“Uzuri wake ndoto yao ni kuwa walimu na wanasema wataolewa wakishamaliza masomo yao. Jambo hilo ni jema na hapo Mungu ndipo atadhihirisha utukufu wake zaidi,” anasisitiza.
Ingetegemewa kwamba katika dunia ya utandawazi, taarifa za kuzaliwa kwa pacha walioungana zingetapakaa kila mahali zikipamba magazeti, redio, luninga na hata mitandao ya kijamii.
Lakini haikuwa hivyo kwa Maria na Consolata. Hakuna chombo chochote kilichopata taarifa ya kuzaliwa kwa pacha hao wa kipekee.
Ulemavu wao ulisababisha wafichwe hadi walipofikisha umri wa kuandikishwa elimu ya msingi katika Shule ya Ikonda na kutafutiwa mlezi wa kuwaangalia, baada ya wazazi wao kufariki dunia wakiwa wadogo.
Habari zao zilianza kufahamika baada ya kuandikishwa darasa la kwanza na kutafutiwa mlezi aliyewalea hadi wakati walipofaulu vizuri mitihani yao ya darasa la saba mwaka 2010.
Mlezi wao, Bestina Mbilinyi alikuwa alifanya hivyo chini ya wamisionari lakini, alikuwa akiishi nao nyumbani kwake Ikonda.
“Niliombwa niishi na watoto hawa kwa sababu kutoka kwangu hadi shuleni sio mbali, nilijengwa choo kinachokidhi maumbile yao na niliishi nao hadi wanamaliza darasa la saba,” alisema wakati akizungumza na Mwananchi wakati walipomaliza darasa la saba.
Baadhi ya wakazi wa mikoa ya Iringa na Njombe wanasema kama watoto hao wasingelelewa chini ya misheni huenda wangepoteza maisha yao au kuuawa kwa imani finyu kuhusu watu walemavu.
Mmoja wa wananchi hao Richard Ndendya mkazi wa Kidabaga anasema mara nyingi walemavu wamekuwa wakichukuliwa kama mkosi kwenye jamii, hivyo huenda kama wasingezaliwa misheni wangepoteza maisha yao aidha kwa kuuawa kutokana na imani finyu au kufariki kawaida, kwa kukosa huduma sahihi.
“Tena tunashukuru Mungu kwa sababu wamisheni waliamua kuwalea watoto vinginevyo huu ushuhuda tunaoupata hivi sasa tusingeupata ushuhuda huu tunaouona,” anasema.
Anasema wanakila sababu ya kulishukuru kanisa la Roman lililojitolea mhanga tangu mwanzo kuwatunza watoto hao ambao leo hii wanaliletea taifa sifa ya kipekee.
Mkazi mwingine wa Kilolo, Eda Kihongozi anasema Tanzania ina kila sababu za kujisifia na kuandaa mazingira mazuri zaidi kwa mapacha hao kufikia ndoto zao kimaisha.
Wanavyolala usiku
Kutokana na namna walivyoungana, ikiwa mmoja atalala kabisa basi mwingine kichwa chake huwa juu juu hivyo hulazimika kuwekwa mto mkubwa ili aweze kuegamea.
“Tunaweza kulala kwa aina nyingi. Anaweza kutangulia Maria mimi nikawa juu au tukabadilishana,”anasema.
Chumbani kwao kuna redio. Kwa kuwa hawapendi kupitwa na jambo lolote linaloendelea nchini na duniani kwa ujumla, huwa wanaiacha redio yao hewani usiku kucha.
Kuungana kwa baadhi ya viungo vyao kumewafanya wapendane zaidi, tofauti na pacha wengine.
Kila mmoja anamuhisi mwenzake, na hilo limewafanya wafurahi na kuhuzunika pamoja.
Chumba wanacholala ni kisafi wakati wote, na wao wenyewe ndio watu wanaosafisha ikiwa ni pamoja na kutandika kitanda kwa ustadi.
Maisha yao
Kiujumla wanaishi maisha ya mazuri kwenye kituo chao cha Nyota ya Asubuhi.
Maria na Consolata wanasema maisha yao ni ya kawaida kama ilivyo kwa watu wengine na kwamba, wanafurahi kulelewa kituo hapo kwa kuwa licha ya kupewa mahitaji yote muhimu, wanapendwa.
Maria anasema hawana wasiwasi kutokana na malezi bora wanayopewa na kikubwa zaidi ni kufundishwa kumcha Mungu.
“Tuna kila sababu za kumshukuru Mungu na masista wanaotulea kwenye kituo hiki kwa kuwa wao ni sababu ya sisi kuishi na kufikia hatua hii kubwa kielimu,” anasema Consolata.
Kwenye nyumba yao waliyojengewa, yupo dada anayewalea, Fransisca Mlangwa, ambaye anasema hajawahi kujuta kuwa mlezi wao.
“Inapotokea wapo mbali nami huwa nawakumbuka, nawaona kama wadogo zangu wa kuzaliwa. Hawa ni mabinti wa kipekee kwa kweli, sijawahi kununa nikiwa nao, mara nyingi huwa wananichekesha na ninaona fahari kuwa mlezi wao,” anasema.
Francisca ni mwanafunzi anayesomea masuala ya mifugo kwenye kituo hicho.
Maria anasema nyumba hiyo imewekwa miundombinu yote muhimu inayowafanya wajisikie vizuri wakati wote wanapokuwa nyumbani.
“Tuna TV na simu ya mkononi ya kisasa hivyo tunasikia na kupata habari mbalimbali zinazoendelea nchini,” anasema Consolata.
Chanzo: Mwananchi

 MATUKIO ZAIDI YA KUSISIMUA BOFYA HAPA 

AJIRA MPYA ZIMETANGWAZWA, BOFYA HAPA
http://studentswagas.blogspot.com/