BALOZI AJERUHIWA KWA KISU
Baada ya kutekeleza shambulio
hilo mhusika alijaribu kutoroka ila maafisa wa polisi walifanikiwa kumkamata.
Balozi wa Marekani nchini Korea
Kusini, Mark Lippert ameshambuliwa na kujeruhiwa kwa kisu usoni na mkononi na
mwanaume mmoja katika jiji la Seoul huko Korea ya Kusini.
Shambulio hilo lilitokea wakati
balozi huyo alipokuwa akielekea kwenye semina jana asubuhi katika mji wa Seoul.
Mwanaume mmoja aliyesikika
akipiga kelele zilizosema Korea Kaskazini na Korea Kusini zinatakiwa kuungana
na vita havitakiwi Korea alimvamia Lippert ambapo alimjeruhi vibaya kwa kisu
usoni na mkononi.
Baada ya kutekeleza shambulio
hilo mhusika alijaribu kutoroka ila maafisa wa polisi walifanikiwa kumkamata.
Mtuhumiwa huyo ametambuliwa na
maofisa hao kuwa ni Kim Ki-jong mwenye miaka 55.
Maafisa wa ngazi ya juu wa
upelelezi wa Korea Kusini wamesema kuwa Kim alikuwa na safari za kwenda Korea
Kaskazini mara 6 mfululizo kati ya mwaka 2006 na 2007.
Kwa mujibu wa shirika la habari
la Daily Mail, madaktari wanaomhudumia Lippert wamesema kuwa mpaka sasa
amepatiwa matibabu katika sehemu za uso na mikono zilizokuwa zimejeruhiwa
vibaya kwa kisu ambapo usoni ameshonwa nyuzi 80.
Waziri Mkuu wa Korea Kusini, Lee
Wan - Koo amesema kwamba amesikitishwa sana kwa kutokea kwa tukio hilo.
Polisi wamesema kuwa Kim ni mmoja
kati ya wanachama wa chama cha Korea kinachotaka muungano baina ya nchi hizo
mbili ambao ndio waliokuwa wameenda kufungua kinywa katika semina ambayo balozi
Lippret alihudhuria jana asubuhi.
Polisi hao wamesema kuwa kisu
ambacho Kim alitumia kumshambulia nacho Lippert kilikuwa na urefu wa inchi 10.
Madaktari wanaomtibu Lippert
wamesema kuwa Lippert ataendelea kubaki hospitalini kwa siku tatu au nne zaidi
ili kuuguza majeraha hayo.
Hata hivyo polisi wamesema kuwa
hili si shambulizi la kwanza kufanywa na Kim dhidi ya maafisa wa kigeni nchini
humo.
Mwaka 2010 Kim alifungwa jela
miaka 3 kwa kufanya fujo katika ubalozi wa Japan nchini humo ambapo alikuwa
akipinga madai ya Japan kuhusu umiliki wa kisiwa cha Dokdo ambacho Serikali ya
Korea na Japan wanamzozo wa juu ya umiliki wa kisiwa hicho.
Shambulio hili limeibua maswali
kadhaa huku wengi wakijiuliza kuwa je, Kim anafanya kazi mwenyewe au
anashirikiana na makundi mengine ya ugaidi ya huko Korea ya Kaskazini.