Chanzo chetu kimeshuhudia moto huo
mkubwa ukiwa umesambaakatika eneo kubwa la safu ya milima hiyo ya Uluguru,
ambapo ilimtafuta mhifadhi wa Uluguru Nature Reserve iliyo chini ya wakala wa
misitu, karani Sekiete, ambaye anakiri pamoja na milima hiyo kuwa salama kwa takribani
miaka mitatu iliyopita bila tatizo la moto, kutokana na elimu zaidi kutolewa na
mashirika mbalimbali na wakala wa misitu, hali imegeuka siku chache zilizopita
baada ya kuzuka kwa moto huo unaosambaa kwa kasi kutokana na ukame na upepo
mkali.
Mhifadhi huyo anasema
wamebaini sababu mbalimbali kuchangia moto na ongezeko la moto katika milima
hiyo, ikiwemo kuona viashiria vilivyoonekana kusababisha, ikiwemo uwindaji wa
wanyama wadogowadogo waliopo maeneo hayo, uchimbaji wa kile kinachoaminika ni
madini, na hata masuala ya kisiasa kwa baadhi ya viongozi kuwakataza wananchi
kuzima kwa kuamini jukumu hilo ni la serikali, taasisi fulani au wakala wa
misitu bila kutambua jukumu hilo ni la kila mtu.
Chanzo chetu kimefika ofisi za mkuu wa
wilaya ili azungumzie jitihada za ziada zinazohitajika na kama wapo watu
waliokamatwa kwa kuanzisha moto huo na kuelezwa kuwa mkuu huyo wa wilaya
Muhingo Rweyemamu ndio kwanza alikuwa ameripoti ofisini, na aliyehusika
kuzungumzia ni katibu tawala wa wilaya, ambaye alikataa kuzungumza lolote kwa
madai hadi moto huo uzimike, huku wananchi wakizungumzia athari za moto huo na
kuwalaani waliosababisha.
Milima ya Uluguru imekuwa
chanzo kikubwa cha maji kwa wananchi wa mikoa ya Morogoro, Pwani na Dar es
Salaam na imekuwa na viumbe hai ikiwemo wanyama na mimea na bionuwai zingine
ambazo hazipatikani kwingineko duniani.