Sunday, December 13, 2015

CCM, Chadema, Waendelea Kukabana Umeya, Uwenyekiti


Mikoani. Vyama vya CCM na Chadema vinaendelea kukabana koo maeneo mbalimbali katika kuwania nafasi ya umeya na uenyekiti wa halmashauri.

Chadema inayoundwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kupambana na CCM kumekuja baada kuzoa viti vingi vya madiwani katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25.

Morogoro
Mgombea wa CCM, Paschal Kihanga ameibuka mshindi wa umeya katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro baada ya kumshinda mpinzani wake, Mabula Lusewe wa Chadema.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Theresia Mahongo jana alisema Kihanga amepata kura 36 wakati Lusewe (4).

Milikiel Mahiku (CCM) aliibuka naibu meya kwa kupata kura 36 akimshinda Juma Temba wa Chadema aliyepata kura nne.

Babati
Diwani wa Babati mkoani Manyara, Mohamed Kibiki (Chadema) amekuwa mwenyekiti mpya wa halmashauri hiyo baada ya kumshinda diwani wa Singe, Martin Hhiya (CCM).

Katibu tawala wa wilaya, Cade Mshamu alisema Kibiki alishinda nafasi hiyo baada ya kupata kura nane wakati Hhiya alipata kura nne.

Mshamu alisema diwani wa Nangara, Elisante Munisi (Chadema) alichaguliwa kuwa makamu mwenyekiti kwa kupata kura nane wakati diwani wa Bonga, Hiiti Q’aambalali (CCM) alipata kura nne.

Wakati huohuo, Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Karatu, Mkoa wa Arusha juzi lilivunjika kutokana na madiwani wa Chadema, kupinga kuteuliwa na kuampishwa kwa diwani wa viti maalumu wa CCM, Sebastian Massay.

Diwani huyo aliteuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC) katika barua iliyoandikwa Novemba 27.

Kwa uteuzi huo, CCM yenye madiwani wanne, itakuwa na madiwani wawili wa viti maalumu na Chadema yenye madiwani 10 itakuwa na wanne wa viti maalumu.

Mgogoro huo, ulianza muda mfupi baada ya katibu tawala wa wilaya, Abbas Kayanda kuanza kutoa utaratibu wa kuapishwa madiwani na jinsi ya kufanyika kikao cha kwanza cha baraza.

Hata hivyo, madiwani wa Chadema walianza kuhoji uwapo wa Massay, ndipo mzozo ulipoanza na kumlazimu katibu huyo kuahirisha kikao cha baraza kwa nusu saa ili madiwani hao wajadili suala hilo.

Diwani Jubilate Mnyenye alisema taratibu zipo wazi za uteuzi wa madiwani, kwani hata katika baraza lililopita CCM ilikuwa na madiwani wanne na kupata kiti kimoja.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Karatu, Moses Mabula alisema amepokea maelekezo ya NEC ya kufuta barua za nyuma na kuteuliwa madiwani wawili wa CCM na wanne wa chadema.