Sunday, December 13, 2015

NEWS: Wafanyabiashara 15 Kuuvaa mkono Wa John Pombe Magufuli


Dar es Salaam. Wafanyabiashara 15 wanakabiliwa na uwezekano wa kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma za kutolipa kodi, baada ya kushindwa kutumia ahueni ya siku saba iliyotolewa na Rais John Magufuli ya kulipa ili kuepuka hatua za kisheria.

Rais Magufuli, alipokutana na wafanyabishara, alitoa nafuu hiyo zaidi ya wiki moja iliyopita, lakini kitendo cha wafanyabiashara hao kutolipa kumeisababishia Serikali kushindwa kukusanya kwa wakati Sh3.75 bilioni wanazodaiwa. Mbali na kuwabainisha wafanyabiashara hao, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pia imetangaza rasmi kuwa itaanza kutoa bure mashine za kielektroniki za kukatia risiti (EFD) kwa wafanyabiashara wote wanaostahili.

Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA, Dk Philip Mpango aliwaeleza wanahabari kuwa hadi jana ni kampuni 28 tu ndizo zilizotii agizo hilo la Rais na kufanikisha ukusanyaji wa Sh10.643 bilioni.

Dk Mpango alisema kuwa muda wa kulipa kodi kwa hiari uliisha Desemba 11, hivyo wafanyabishara hao 15 ambao wameshindwa kabisa kulipa kodi katika kipindi hicho “wasubiri cha moto” kwa kuchukuliwa hatua kali za kisheria kwa kuwa ni lazima mapato ya Serikali yalipwe.

“Hata hizo siku saba walizokuwa wamepatiwa tayari walikuwa wameshavunja sheria, hivyo wale waliolipa kwa wakati wamesamehewa kupelekwa mahakamani, lakini ambao hawajalipa watashtakiwa na kupigwa faini,” alisema Dk Mpango bila kubainisha kiwango cha adhabu.

Alisema baadhi ya wafanyabiashara hao walienda “kulalamika lalamika”, lakini TRA haitawasamehe kwa kuwa kodi hizo zinahitajika kufanikisha utoaji wa huduma kwa wananchi. Dk Mpango alibainisha kuwa kati ya fedha zilizokusanywa katika kipindi hicho, Sh4.16 bilioni kinatoka kampuni 13 ambazo zimelipa kodi yote iliyokuwa imekadiriwa, huku Sh2.2 bilioni zikitoka katika kampuni 15 zilizotoa sehemu ya mapato waliokuwa wakidaiwa.

Sanjari na kampuni hizo, bosi huyo mpya wa TRA alisema kampuni ya bandari kavu ya Azam ICD ililipa kiasi cha Sh4.17 bilioni kama dhamana kati ya Sh12.6 ya kodi iliyokuwa imekwepwa katika sakata la upotevu wa makontena 329.

Katika kuhakikisha wote waliokwepa kodi kwa kuondoa makontena bandarini kinyume na sheria na taratibu za forodha wanalipa mapato hayo ya Serikali, TRA imefungua akaunti maalumu Benki Kuu ya Tanzania (BOT) ijulikanayo kama ‘commissioner for customs and excise-Container Account namba 9921169785 itakayorahisisha ukusanyaji huo.

“Wale wote ambao wanapaswa kulipia kodi pamoja na adhabu ya kuondosha makontena bandarini kinyume na taratibu wanaelekezwa kutumia akaunti hii kulipa kiasi chote wanachodaiwa,” alisema Dk Mpango.
Kwa kipindi cha hivi karibuni, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amefanya ziara ya kushtukiza mara mbili bandarini na kugundua uwepo wa mtandao wa ufisadi uliosababisha upotevu wa awali makontena 349 na mara ya pili makontena 2,431 yaliyotolewa bila kulipa ushuru.

Mpaka sasa tayari Rais Magufuli ameshamsimamisha kazi mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Bandari (TPA), Awadhi Massawe na kamishna mkuu wa TRA, Rished Bade kupisha uchunguzi wa masakata hayo, huku akiivunja Bodi ya bandari.

Ili kuongeza ufanisi wa bandari kavu nchini, Dk Mpango alisema ofisi yake inaanza kupitia upya utaratibu wa kutoa leseni za ICD pamoja na usimamizi, kazi aliyosema itaondoa ‘uozo’ wote katika vituo hivyo vya dhamana za forodha.

“Mamlaka itaanza kupiga picha makontena yote yanayopita bandarini hapo tofauti na awali ambako yalikuwa yanapigwa picha machache kama sampuli,” alisema.
Ili kwenda na kasi ya utoaji mizigo na upigaji picha, alisema TRA inafanya utaratibu wa kuongeza mashine za kukagulia mizigo hiyo ziitwazo “scanner”.
EFD bure
Katika kutii agizo jingine la Rais, TRA imetangaza kuwa wafanyabiashara takriban 200,000 wenye sifa za kupatiwa EFD, watapewa badala ya utaratibu wa zamani wa kuwakopesha.

Alisema awali fedha za mkopo wa mashine hizo zilikuwa zinarudishwa kupitia marejesho ya mapato yao kwa mamlaka.

“Kwa sasa bado tunafanya uchambuzi wa wafanyabiashara wanaotakiwa kupatiwa mashine hizo. Tunaangalia tutagawaje mashine hizo siyo zote kuziweka Dar es Salaam wakati na mikoani inabidi tuzipeleke za kutosha,” alisema Dk Mpango.

Pia, kiongozi huyo wa zamani wa Tume ya Mipango, aliwataka watumishi wote kukamilisha ujazaji fomu za kutangaza mali zao kwa kuwa zimesalia siku mbili la sivyo sheria na taratibu za kiutawala zitachukuliwa kuwaadhibu.

Utilities:
Wafanyabiashara 15 ambao hawajatii agizo la Rais.
1. Ahmed Tawredkariako Areadar: Sh59.2 milioni.
2. CLA Tokyo Ltd: Sh77.5 milioni.
3. Farida Salem: Sh75.3 milioni.
4. Juma Abdul: Sh190.1 milioni.
5. Libas Fashion: Sh52.9 milioni.
6. Rushywheel Trye Centre Co Ltd: Sh1.8 bilioni.
7. Said Hamdan: Sh68.3 milioni.
8. Said Ahmed Said: Sh68.7 milioni.
9. Salum Continental Co Ltd: Sh151.1 milioni.
10. Salum Link Tyres: Sh343.4 milioni.
11. Simbo Kimaro: Sh69.2 milioni.
12. Snow Leopard Building Material Ltd: Sh93.9 milioni.
13. Swaleh Mohamed Swaleh: Sh34.6 milioni.
14. Tybat Trading Co Ltd: Sh598.6 milioni.
15. Nasir Mazrui: Sh70.1 milioni.

Chanzo Mwananchi