Sunday, April 3, 2016

Leicester alama 7 juu, Man U nafasi ya 5


Leicester waliimarisha nafasi yao ya kutwaa kombe lao la kwanza la ligi kuu ya Uingereza EPl walipoibana Southampton kwa bao moja kwa nunge.
Nahodha wa The Foxes Wes Morgan alitumia vyema pasi safi ya Christian Fuchs na kuiweka Leicester alama 7 kileleni mwa jedwali la ligi kuu huku wakiwa wamesalia na mechi 6 kukamilisha msimu huu kwa kishindo.
Vijana wa Claudio Ranieri wanaweza kunyanyua kombe la msimu huu iwapo watashinda mechi nne kati ya 6 zilizosalia.
Hata hivyo matokeo ya leo yalikuwa ya kipekee kwa nahodha huyo wa Leicester City kwani bao hilo ndilo lililokuwa bao la kwanza la Morgan msimu huu.
Southampton watajilaumu wenyewe kwani Sadio Mane kwa wakati mmoja alionekana kuwa fursa nzuri ya angalau kusawazisha hususan baada ya kummwaga Kasper Schmeichel, lakini kombora lake likazimwa na Danny Simpson.
Leicester waliendeleza msururu mpya wa ushindi wa bao moja kwa nunge katika mechi 5 kati ya 6 za hivi punde.
Matokeo ya wapinzani wao wakuu Tottenham ya sare dhidi ya Liverpool siku ya Jumamosi bila shaka liliwapatia motisha kujikakamua hii leo.
Licha ya kichapo hicho ugenini,Southampton wamesalia katika nafasi ya saba.
Awali mashabiki wote walioshuhudia mechi hiyo walipewa kopo la pombe au kaimati kuadhimisha siku ya kuzaliwa ya mmiliki wa klabu hiyo.
Katika mechi nyengine iliyokuwa ikitazamiwa na wengi, bao la Anthony Martial lilitosha kuipa Manchester United ushindi muhimu waliohitaji dhidi ya vibonde wao wa jadi Everton.
Katika hafla ya kuadhimisha nyota wao wa zamani Sir Bobby Charlton, vijana wa kocha van Gaal walihitaji ushindi na alama tatu ilikuiweka hai matumaini yao ya kumaliza katika nafasi 4 za kwanza katika EPL.
Na baada ya kukosa bao katika kipindi cha kwanza, Man united walirejea kutoka mapumzikoni kwa kishindo.
Martialalitumia vyema pasi safi ya Tim Fosu-Mensah na kuiacha Everton ikijiliwaza baada ya kupoteza mechi yao ya tatu mfululizo katika ligi kuu ya Uingereza.
Phil Jagielka alikosa nafasi nzuri ya kichwa na kisha kombora lililokolewa na kipa David De Gea.
Kufuatia ushindi huo muhimu vijana wa Van Gaal sasa wapo alama 1 tu nyuma ya timu inayorodhoshwa ya nne Manchester City.