Tuesday, May 31, 2016

Zitto, Lissu na Mdee wafukuzwa bungeni

VURUGU zilizotokea bungeni Januari 27 mwaka huu, wakati wa kutangaza uamuzi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kurusha matangazo moja kwa moja (live) baadhi ya vipindi vya Bunge, zimesababisha baadhi ya wabunge wa kambi ya upinzani, kufukuzwa bungeni.
Akisoma maazimio ya Bunge mjini hapa jana jioni, Mwenyekiti wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, George Mkuchika alitaja adhabu tatu ambazo zote zinahusu kufukuzwa kwa wabunge hao, lakini kwa uzito tofauti.
Waliopewa adhabu kali zaidi ni Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, ambao wamepigwa marufuku kuhudhuria vikao vyote vya Bunge la Bajeti linaloendelea kuanzia jana pamoja na Bunge lijalo.
Adhabu ya kati imekwenda kwa Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, Mbunge wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto na Mbunge wa Kawe jijini Dar es Salaam, Halima Mdee.
Hao wanne wamepigwa marufuku kuhudhuria vikao vyote vya Bunge la Bajeti kuanzia jana. Adhabu ndogo imekwenda kwa Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche. Yeye amepigwa marufuku kuhudhuria vikao 10 mfululizo vya Bunge la Bajeti kwa sababu alikutwa na kosa moja, lakini alitoa ushirikiano na kuitikia mwito wa Kamati.
Baadhi ya wabunge waliojadili hoja ya Kamati hiyo, kabla ya Bunge kutoa azimio, walitaka adhabu kama hizo zichukuliwe haraka, mara mbunge anapofanya makosa, badala ya kuchukua muda, kama ilivyofanyika. Hata hivyo, Mkuchika alisema walilazimika kwanza kuwapa muda wajirekebishe na muda wa kujitetea, kabla ya kuchukua hatua hizo.
Alisema hatua hizo zimetokana na sheria inayotoa haki na madaraka ya Bunge.