Monday, May 8, 2017

Miili ya waliokufa ajalini Muheza yaanza kutambuliwa

Muheza. Miili ya abiria waliokufa katika ajali iliyotokea juzi saa 2.45 usiku baada ya basi aina ya Coaster walilokuwa wamepanda kuligonga lori wameanza kutambuliwa kufuatia ndugu zao kujitokeza katika hospitali ya teule wilayani hapa.



Basi aina ya Coaster lililokuwa likitokea Jijini Tanga kuelekea mjini Muheza liligonga lori aina ya Scania lenye tela lililokuwa limeegeshwa pembeni katika kijiji cha Lusanga, barabara kuu ya Tanga-Segera na kusababisha abiria wanne kufa na wengine 13 kujeruhiwa.

Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mwanasha Tumbo aliiambia Mwananchi kwamba hadi jana mchana miili ya abiria wawili kati ya wanne waliokuwa wamehifadhiwa katika hospitali hiyo ilikuwa imetambuliwa na ndugu zao.

Aliwataja waliokufa na kutambuliwa na ndugu zao kuwa ni Ummy Amiri (28) aliyekuwa mkazi wa Kijiji cha Tingeni pamoja na Nassib Salim (18) aliyekuwa mkazi wa Kitongoji cha Ngorongoro Wilayani hapa.

Majeruhi wa ajali hiyo ambao wote wanapata matibabu katika hospitali ya teule kwa mujibu wa mkuu huyo wa wilaya ni Abdallah Majid (37), Mlondwa Guge (44), Twahiru Sebarua(35) na Shaaban Abbas (21).

Majeruhi wengine ni Festo Asilia (35), Abdillah Fungo (32), Ali Mohamed (30), Isihaka Hassan (27), Ibrahim Bilal mtoto anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka mitatu hadi mitano, Magreth Tito (35) na Ummy Omary (23).

MATUKIO ZAIDI YA KUSISIMUA BOFYA HAPA