Wednesday, May 17, 2017

OCD wa Polisi auawa kikatili

MKUU wa Polisi wa Wilaya (OCD) ya Uvinza mkoani Kigoma, Amedeusi Malenge, ameuawa na watu wasiojulikana nje ya nyumba yake Kinyerezi, jijini Dar es Salaam.
Mkuu huyo wa polisi, imeelezwa, alikuwa likizo jijini akitokea Kigoma na alipatwa na umauti saa tatu usiku juzi, baada ya kupigwa na kitu kizito na watu wasiojulikana, alipokuwa anatoka katika matembezi.
Habari za kuaminika zinasema Malenge ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya (OC-CID) ya Kibaha kabla yakuhamishiwa Uvinza, alikutana na watu ambao walikuwa wamewateka walinzi wa nyumba yake iliyoko Kinyerezi wakati akirudi kutoka katika matembezi, ambao walimuua.
“Taarifa za awali tulizopata ni kwamba alikuwa anatoka kula maana pale anapoishi haishi na mke,” alisema mmoja wa mtu aliyewahi kufanya kazi na marehemu.
"Ndipo alipokuwa anarudi akawakuta walinzi wake wametekwa nje karibu na nyumbani kwake, akasimamisha gari na kushusha kioo na kuuliza kulikoni.
"Wakati anauliza wale watu walimvamia katika gari lake na kumpiga kichwani na kitu kizito ambapo alifariki papo hapo."
Chanzo: Nipashe

Matukio zaidi ya Kusisimua Bofya hapa