Dr. Harisson Mwakyembe
“Ni
utashi wa Mheshimiwa Rais kuamua kuwapanga wasaidizi wake kwa namna anayoona
inafaa.
Arusha. Siku mbili baada kukabidhiwa ofisi na
aliyekuwa Waziri wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta, waziri ambaye ameteuliwa
kushika nafasi hiyo, Dk Harisson Mwakyembe amewataka Watanzania kuondoa hofu ya
kuhamishwa kwake kutoka Wizara ya Uchukuzi, huku akisisitiza kuwa hana nia ya
kugombea urais.
Dk
Mwakyembe aliwataka wananchi kuondoa hofu kwa sababu utendaji aliouonyesha
akiwa Wizara ya Uchukuzi, atauhamishia wizara yake mpya.
Akizungumza
katika mahojiano maalumu na gazeti hili muda mfupi baada ya kuapishwa na Spika
wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala), Daniel Kidega, Mwakyembe alisema utendaji
aliouonyesha katika wizara aliyokuwamo awali zamani, ndiyo uliomshawishi Rais
Jakaya Kikwete kumhamishia Wizara ya Afrika Mashariki ili kuongeza kasi ya
utekelezaji wa masuala ya jumuiya hiyo.
“Watanzania
wanapaswa kuondoa kasumba ya kutaka anayefanya vizuri katika nafasi yake
kuendelea kubaki hapo hapo. Hapana! Anayefanya vizuri sehemu moja ni vyema
akahamishiwa sehemu nyingine ili akafanye vizuri huko pia,” alisema Mwakyembe
na kuongeza:
“Ni
utashi wa Mheshimiwa Rais kuamua kuwapanga wasaidizi wake kwa namna anayoona
inafaa. Naamini utendaji wangu Wizara ya Uchukuzi ndiyo umesababisha
nihamishiwe Afrika Mashariki ili niuendeleze huku pia.”
Kauli
ya Waziri Mwakyembe inakuja siku chache baada ya kutolewa kwa maoni ya wananchi
yaliyoonyesha kutoridhishwa na uamuzi wa Rais kumbadilisha kutoka Wizara ya
Uchukuzi kwenda Afrika Mashariki akibadilishana na Sitta aliyekwenda Wizara ya
Uchukuzi.
Sina
nia kugombea urais 2015
Akizungumzia
malengo yake kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka huu, Mwakyembe alisema:
“Akili na malengo yangu yote kwa sasa ni kutekeleza majukumu yangu kama Waziri
wa Afrika Mashariki. Sina nia ya kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu ujao. Hilo
nawachia wenye nia hiyo,” alisema.
Tayari
wanachama kadhaa wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wametangaza au kutajwa kwenye
mbio hizo za urais.
Faida
ya ushirikiano wa EAC
Akizungumzia
faida za EAC, Waziri Mwakyembe alisema muda umefika sasa umma wa Afrika
Mashariki uanze kupata faida ya moja kwa moja ya ushirikiano kati ya nchi
wanachama za Tanzania, Rwanda, Burundi, Kenya na Uganda akitaja nafuu ya
gharama za usafiri kutoka nchi moja kwenda nyingine kuwa miongoni mwa maeneo
muhimu ya kuangaliwa.
“Miaka
15 sasa imepita tangu kufufuliwa kwa jumuiya hii, lakini bado ni ghali kusafiri
kwa ndege kati ya Dar es Salaam na Nairobi, Kampala, Bujumbura na Kigali
kulinganisha na Johannesburg, Afrika Kusini, India au Dubai,” alisema.
Mwakyembe.