“Yaani ni Mungu tu, hivi sasa tungekuwa tunazungumza mengine kuhusu Mheshimiwa Chenge, wafuasi wa Chadema wangemuua,” alisema shuhuda wa tukio hilo aliyezungumza na gazeti hili kwa sharti la kutoandikwa jina lake gazetini na kuongeza:
“Mikutano yote iliisha salama na wafuasi wa Chadema wapatao 2,000, wakawasindikiza viongozi wao kwenda kwenye ofisi za Chadema zilizopo Mwisho wa Lami, kandokando ya Barabara ya Maswa- Lamadi,” alisema shuhuda huyo na kuendelea kuongeza kuwa walipofika kwenye ofisi hizo, waliendelea kuimba na kushangilia na kutawanyika mpaka barabarani.
“Ghafla msafara wa Chenge ukafika eneo hilo huku muziki ukisikika kwa sauti kubwa ndani ya gari moja, wafuasi wote wa Chadema wakiwa wameshika mawe wakauzingira na kuanza kuzomea. Mara Chenge na wafuasi wake wakateremka chini, hapo ndipo kiliponuka.
“Mtu mmoja aliwaamrisha wafuasi wa Chadema kuanza kuwapiga mawe watu wote, akiwemo Chenge, kukatokea bonge la mtiti, Chenge na wenzake wakawekwa ‘mtu kati’ na kutaka kushushiwa kichapo.
“Katika kujihami, mtu mmoja aliyekuwa kwenye msafara wa Chenge aitwaye Ahmed Ismail alifyatua risasi tatu hewani, ndipo wakapata upenyo wa kukimbia baada ya wafuasi wa Chadema kutawanyika.
“Mkanganyiko uliopo ni kwamba CCM wanasema Chadema ndiyo waliowavamia, Chadema nao wanasema CCM ndiyo waliowavamia, hivyo hali ni tete. Tunaendelea kulichunguza tukio hilo,” alisema Kamanda Gemini na kuongeza:
“Wanasiasa wajifunze kupambana kwa hoja wawapo kwenye majukwaa ya siasa lakini siyo kupigana kwa mawe au bastola.”
Kamanda huyo aliongeza kuwa baada ya kufanya uchunguzi, walibaini kwamba bastola iliyotumika, ilikuwa ikimilikiwa kihalali na Ahmed na kwamba hakukuwa na mtu yeyote aliyejeruhiwa.