Jeshi
 la polisi Mkoani Simiyu Linamshikilia Chigila Gilala mkazi wa kijiji 
cha Bukingi Kata ya Malampaka Wilayani Maswa (45) Kwa kosa la kukutwa na
 Viungo vinavyodhaniwa kuwa vya binadamu likiwemo Fuvu la Kichwa.
Mtuhumiwa
huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM katika kijiji hicho na Mganga wa tiba
asili alikamatwa nyumbani kwake, baada ya kuwepo kwa taarifa kuwa  alikuwa
amewahifadhi majambazi kwa ajili kugangwa (kuzindikwa).
 
 
 Akitoa
taarifa kwa waandishi wa kamanda wa  jeshi la polisi Mkoani Simiyu Gemini
Mushy alieleza kuwa tukio hilo la kukamatwa kwa mwenyekiti huyo lilitokea Mei 9
mwaka huu  majira ya saa 11 jioni katika kijiji hicho.
Kamanda
Mushy alisema kuwa askari wakiongozwa na mkuu wa upelelezi katika wilaya ya
Maswa walipata taarifa kutoka kwa raia wema kuwepo kwa majambazi nyumbani kwa
mganga huyo, kuwa alikuwa amewahifadhi kwa ajili ya kuwazindika.
Alisema
baada ya kupata taarifa hizo walifanya msako nyumbani kwa mwenyekiti huyo,
ambapo  alibainisha kuwa walianza kufanya upekuzi ndani na nje ya nyumba.
“Wakati
wakifanya upekuzi huo walikutana na mfuko wa sandarusi ukiwa chini ya lundo la
kuni nje ya nyumba  ya mwenyekiti huyo na katika mfuko huo kulipatikana
fuvu la kichwa pamoja na mifupa ya mikono au miguu vinavyodhaniwa kuwa ni
viungo vya binadamu” Alisema Mushy.
Kamanda
alieleza kuwa jeshi hilo linaendelea kufanya uchunguzi kama kweli viungo hivyo
ni vya binadamu na kama anahusika na uwepo wa viungo hivyo kutokana na
 kukutwa nje ya nyumba yake.