Polisi mkoani kilimanjaro, imemshikilia kwa zaidi ya saa tatu, mgombea ubunge wa Jimbo la Vunjo, kupitia chama cha Mapinduzi (CCM), Innocent Melek, baada ya kudaiwa kumtishia kwa bastola, muongoza watalii, Oscar Mosha (28), akiwa katika klabu ya usiku ya Pub Alberto ya mjini Moshi. Meleck (32), anadaiwa kufanya tukio hilo, akitumia bastola aina ya Bereta, iliyosajiliwa kwa namba H 56420, usiku wa Oktoba 2,  akiwa ameongozana na baadhi ya wapambe wake.

Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Fulgence Ngonyani, aliiambia Nipashe jana kwa njia ya simu kwamba, mgombea huyo alikuwa amekwenda kwenye klabu hiyo kwa ajili ya starehe na wakati akiwa ndani  alifuatwa na mmoja wa wateja wa klabu hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Oscar ambaye alimweleza kuwa ameegesha gari lake vibaya na kuzuia magari mengine kutoka, jambo lililomuudhi. Ni kweli tukio hilo limetokea juzi saa 7:00 usiku katika klabu maarufu ya Pub Alberto, na huyo Innocent aliisalimisha bastola yake kituo kikuu cha polisi mjini Moshi, baada ya kufikishwa hapo.  

Tumewahoji na tumewaachia kwa masharti ili kupisha uchunguzi zaidi, alisema Kamanda Ngonyani. Alisema, Innocent alipohojiwa na polisi kuhusu madai hayo, alidai kupigwa na kuumizwa sehemu ya jicho lake na hivyo alipatiwa fomu namba tatu ya matibabu (PF3) na kwenda kutibiwa katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Kilimanjaro (Mawenzi). Wakati mgombea huyo akidai kupigwa, mlalamikaji alidai kutishiwa kwa silaha na Innocent baada ya kumtaka akaliondoe gari lake ili apishe gari jingine lililokuwa likitaka kuondola eneo hilo.

 Chanzo: Nipashe

 
Top