WATU 17 wakazi wa kijiji cha Kyanyamaswa katika kata ya Barraki wilayani Rorya mkoani Mara wamekamatwa na Polisi Kanda Maalumu ya Tarime Rorya kwa tuhuma za mauaji ya wanawake wawili vikongwe.
Vikongwe hao, Nyakorema Warioba (66) na Ghati Ndege (67) waliuawa kwa kuwapiga na kisha kuwaingiza ndani ya nyumba zao zilizoezekwa kwa nyasi na kuzichoma moto na kusababisha vifo vyao kwa madai ya imani za kishirikina.
Kamanda wa Polisi Tarime Rorya, Andrew Satta alisema mauaji hayo yalifanywa Aprili 11, mwaka huu baada ya kundi la watu waliokuwa na silaha za jadi, mapanga na marungu kuvamia miji ya Nyakorema na Ghati na kisha kuwakamata wanawake hao na kuwashambulia kwa silaha hizo za jadi na kisha kuwaingiza ndani ya nyumba zao zilizoezekwa kwa nyasi na kuziwasha moto na kuwateketeza na kusababisha vifo vyao wote wawili.
Kamanda Satta alisema chanzo cha mauaji hayo inadaiwa ni imani za kishirikina, kwani watuhumiwa wanadaiwa kutekeleza mauaji hayo kutokana na kuwatuhumu Nyakorema na Ghati kuwa walihusika na kifo cha ndugu yao Nyamhanga Ryoba ambaye alifariki jijini Mwanza.
“Tunawahoji watuhumiwa hao na tunatarajia kuwafikisha mahakamani wakati wowote ule baada ya kukamilisha uchunguzi,” alisema Kamanda Satta.