Mtuhumiwa Isaac Emire (katikati)
akiongozwa na askari kuelekea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha
kujibu mashtaka ya kesi hiyo jana.
MKAZI wa Olasiti Jijini Arusha, Isaac Emily (40), amepandishwa
kizimbani kwa kumtolea maneno ya dharau na kumdhihaki Rais John Magufuli
katika mitandao ya kijamii. Alisomewa mashitaka jana na Mwendesha
Mashitaka wa Polisi, Gaudencia Masanja mbele ya Hakimu Mfawidhi wa
Mahakama ya Mkoa wa Arusha, Augustino Rwezile.
Katika mashitaka hayo, Emily amedaiwa kutenda kosa hilo Machi 17
mwaka huu kinyume na sheria ya mitandao namba 16 kifungu namba 14 ya
mwaka 2014. Masanja alidai kuwa, siku hiyo mshitakiwa alisambaza ujumbe
wa uongo katika mitandao ya kijamii wenye lengo la kumdharau, kumdhihaki
na kumtolea maneno Rais Magufuli yenye lengo la kumdhalilisha.
Alidai kuwa ujumbe huo ulisomeka, ”Hizi ni siasa za maigizo halafu
mnamfananisha huyu bwege na Nyerere wapi bwana.’’ Mshitakiwa huyo
alikana kutenda kosa hilo ambapo Mwendesha Mashitaka aliomba Mahakama
isitoe dhamana kwa mshitakiwa huyo, kwa maelezo kuwa ingawa dhamana ni
haki yake ya msingi, lakini usalama wake utakuwa shakani kwani watu
wengi wamekerwa na ujumbe huo na pia akiwa nje anaweza kuvuruga
ushahidi.
Hata hivyo, Emily hakukubaliana na madai ya Mwendesha Mashitaka na
kusema ana uhakika hataingilia upelelezi wa kesi hiyo kwa sababu simu
zake zote ziko mikononi mwa Polisi, hivyo madai ya kusema ataingilia
upelelezi si ya kweli. Mtuhumiwa pia alijitetea kuwa maisha yake
yatakuwa salama endapo atapata dhamana, hivyo kuiomba mahakama impe
dhamana.
Chanzo: HabariLeo