GEITA: MTU mmoja aliyefahamika
kwa jina moja la Mlinda Kioga (38) mkazi wa Kata ya Majengo, Kahama
mkoani Shinyanga amekutwa amenasa mlangoni mwa nyumba ya mganga wa
kienyeji, tukio lililohusishwa na imani za kishirikina.
Inadaiwa mtu huyo alikwenda katika
nyumba hiyo Julai 27, mwaka huu kwa shida ambazo hazikufahamika na
akapokewa na mkewe kabla ya mgeni huyo kuomba hifadhi ya kulala, ambapo
alioneshwa chumba cha kulala.
Mashuhuda wanasema kesho yake asubuhi,
wakati wakipita eneo hilo, mtu huyo alipiga kelele kuomba msaada wa
kumnasua, lakini walipojaribu kumsaidia walishindwa. Inadaiwa mgeni huyo
alitoka usiku kwa lengo lisilofahamika, lakini akajikuta ameganda
mlangoni hadi kesho yake.
“Nilipofika mlangoni niliona giza nene,
sikuweza kurudi chumbani wala kutoka nje, ilibidi nijishikize kwenye
mlango hadi kulipokucha, nimekesha nimesimama kama unavyoona, sikuweza
hata kuchuchumaa wala kuegesha ubavu wangu, naombeni tu msaada wenu,”
alisema Kioga akiwa mlangoni hapo.
Baada ya kushindwa kumnasua, mashuhuda
hao waliomba msaada wa mjumbe wa nyumba kumi, Helena Joel ambaye naye
alishangazwa na tukio huku akimtaja mganga huyo kuwa ni mzee Maziku
Makwaya. Yeye ndiye aliyewaita polisi waliofanikiwa kumtoa mtu huyo
mlangoni.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ASP
Murilo Jumanne amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kama
chombo cha usalama, hakiamini imani za kishirikina.