Manyara: Afisa Uchunguzi wa
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), Wilaya ya
Kiteto mkoani Manyara, Evangeline Samson (pichani) aliyeuawa kwa
kuchinjwa na watu wasiojulikana akiwa nyumbani kwake, undani wa kifo
hicho umesimuliwa, Chanzo chetu kinakupa zaidi.
Marehemu alifikwa na mauti hayo, usiku
wa Julai 24, mwaka huu ndani ya nyumba yake iliyopo katika Mtaa wa
Bomani, Manispaa ya Kiteto.
Chanzo cha mauaji hayo kinatajwa kuwa ni
wivu wa kimapenzi lakini bado suala hilo lipo chini ya uchunguzi wa
polisi kuwabaini wauaji hao na tayari wameshakamatwa watuhumiwa watano.
Ibada ya Mazishi
Kwa mujibu wa chanzo cha karibu, kabla
ya kukutwa na mauaji, marehemu alikuwa amekaa sebuleni ambapo zilikutwa
glasi mbili za pombe kali na sahani mbili za wali na nyama ulioliwa na
kubakizwa.
“Mezani kulikutwa glasi mbili za
kinywaji kikali. Sasa hatujui kama marehemu alikuwa anakunywa kinywaji
hicho na mtu mwingine au la,” alisema mmoja wa mashuhuda ambaye hakutaka
jina lake liandikwe gazetini.
Naye jirani mmoja ambaye pia aliomba
hifadhi ya jina lake gazetini, alisema siku moja kabla ya tukio hilo,
marehemu alikuwa akilalamika kutojisikia vizuri.
“Nilipomuuliza kama anaumwa, alisema
haumwi bali anajisikia kama amefanya jambo baya ambalo litamuingiza
hatiani. Nilimuuliza kama aligombana na mtu wake wa karibu, akasema
hakuna.
“Kusema ukweli mpaka inafika usiku,
marehemu hakuwa sawa. Nadhani kiroho alikiona kifo chake ila alishindwa
kukitafsiri,” alisema jirani huyo.
Wafanyakazi waliokuwa wakifanya kazi na
marehemu, walisema wanaamini kuna kisasi kilichosababisha kifo cha
mwenzao lakini hawajui kama ni kuhusu mapenzi au kazi.
“Kuna kisasi tu lakini vigumu kujua kama
ni mapenzi au kazi. Polisi wanachunguza, watasema walichokipata. Ila
kusema ukweli mwenzetu amekufa kifo kibaya sana,” alisema mfanyakazi
mmoja.
Wakati wa kuaga mwili wa mwanamke huyo,
kila mtu alikuwa akisema lake lakini walichokilenga wengi ni kuwa,
mauaji hayo yana kisasi ndani yake.
Chanzo chetu kilipomtafuta
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, ACP Francis Massawe, alithibitisha
kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa, wanawashikilia watuhumiwa watano.
Marehemu ameacha mtoto mmoja, Ethani (7). Alitarajiwa kuzikwa Jumatano iliyopita nyumbani kwao, Ilongero, Singida.
Hadi anakutwa na mauti, marehemu alikuwa akiishi peke yake baada ya kuachana na mume wake wa ndoa miaka michache iliyopita.
Chanzo: Uwazi