Hatimaye mgombea Urais kwa tiketi ya chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk, John Magufuli, ameibuka hadharani na kuzungumzia tatizo la kuwapo kwa baadhi ya wafuasi wa Chama chake kuhujumu kwa kuunga mkono harakati za upinzani.
Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli
Akizungumza kwenye
viwanja vya Zimbiilo, Wilaya ya Muleba Kusini jana, Magufuli alisema anatambua
kuwapo kwa baadhi ya wanaCCM wanaojionyesha kumuunga mkono nyakati za mchana
lakini inapofika usiku hubadilika na kuwaunga mkono wapinzani.
“Naomba na nyinyi
msiniangushe maana wengine mchana mnakuwa CCM, usiku mnahamia vyama vingine,
mimi nina moyo kama nyie jamani msiponichagua nitakwazika sana Wanamuleba,”
alisema Magufuli.
Hivi sasa, Magufuli
amekuwa akichuana vikali na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anaeywakilisha pia muungano wa vyama
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya NLD, NCCR-Mageuzi na Chama
cha Wananchi (CUF). Wote wawili wamekuwa wakivutia maelfu ya wananchi karibu
katika kila mikutano yao ya kampeni kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 25.
Kadhalika, Mwenyekiti
wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Abdalah Bulembo, alizungumzia pia tatizo hilo la
kuwapo kwa wanachama wa CCM ambao wamekuwa wakisaidia wka kificho kampeni
za mgombea urais kwa tiketi ya Ukawa, Lowassa.
Bulembo alifichua hayo
wakati akizungumza kwenye mkutano wa kumnadi Dk. Magufuli katika Jimbo la
Bukoba Vijijini.
Akieleza zaidi,
Bulembo alisema ana ushahidi kwamba ziara ya Lowassa mkoani humo iliratibiwa na
baadhi ya viongozi wa chama hicho na hivyo akawataka kuamua moja, ama
kuitumikia CCM kwa dhati au kuondoka CCM mara moja na kumfuata Lowassa.
“Msidhani hatuwafahamu. Mikakati yote na namna mnavyofadhili Ukawa na Lowassa
tunafahamu, tena tunawafahamu kwa majina na nawaambia ole wenu... msipoondoka wenyewe,
tutawafukuza baada ya Dk. Magufuli kushinda,” alisema Bulembo ambaye pia ni
Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM.
“Anayempenda Lowassa
na Ukawa avue magwanda ya CCM na awafuate huko. Hatutaki watu ambao mchana ni
CCM usiku ni Lowassa… hili ni gari kubwa. Wengine wanashuka, wengine
wanapanda,” alisema Bulembo.
Alisema yeyote mwenye
kinyongo na CCM hafai kubaki ndani ya chama hicho kwa sababu (chama hicho) kina
wanachama wengi na hakiangalii uwezo wa mtu kifedha.
“Tunawajua
mnaomng’ang’ania Lowassa. Lakini nawahakikishia kuwa mtalia baada ya uchaguzi
wa mwaka huu... mnajifanya CCM lakini mnafadhili upinzani, mwisho
wenu unakuja,” alisema Bulembo.
Chanzo: Nipashe