Photo: "BONGO DAS'LAAM"
Imechapwa gazeti la SANI
Mtunzi: Kizaro Mwakoba.

SEHEMU YA KWANZA:
Taarifa za maisha bora na mazuri yaliyokuwepo JIJINI DAR ES SALAAM zilimvutia sana kijana AYUBU na kuingiwa na tamaa za kwenda kutafuta maisha jijini humo. Rafiki yake aliyekwenda huko miezi michache tu iliyopita akarejea akiwa amependeza na kuonekana kufanikiwa kimaisha. Hivyo Ayubu hakuona sababu ya kendelea kubakia kijijini kwao Lusanga kule mkoani Tanga kuteseka na umasikini. Alichofanya ni kupanda gari na kuelekea jijini Dar es salaam pasipo hata kuaga nyumbani kwao.
*****
Kelele za vijana waliotaka kumsaidia zilimchanganya sana, akakumbuka maneno ya watu kuwa pale jijini kulikuwa na vibaka. Alipata wazo la kukumbatia begi lake kwa umakini. alivuta hatua kadhaa na kusimama akiangalia huku na kule, akajikuta akitoa tabasamu na kujiona shujaa kwa kufika jijini DareSalaam.
Swali likabaki je aelekee wapi? na huyo rafiki yake angempataje? Hakujua amuulize nani kwasababu kila mtu alionekana kuwa bize na mambo yake. Pale aliposimama alipita kijana mmoja mtanashati, Ayubu akaona yule mtu alikuwa anafaa kumuelekeza mahali alipokuwa akiishi rafiki yake, akamsimamisha kijana yule
"Samahani kaka, naomba kuuliza"
"Sory nawahi sehemu" alijibu yule kijana na kuondoka pasipo kumsiliza Ayubu. Ayubu akamuendea muuza maji na kumuuliza.
"Habari yako kaka?"
"Safi broo, nikutolee makubwa au madogo?"
"Hapana ndugu, naomba nikuulize kitu"
"Kuuliza ni mia tano. unayo?"
"Sawa.... hii hapa" Ayubu alijibu na kutoa shilingi mia tano na kumkabidhi yule kijana.
"Ok. uliza "
"Unafahamu anapokaa Kondo?"
"Kondo! yeye ni nani hapa Dar?"
"Alikuwa anaishi kwenye kijiji chetu"
"Wewe ni mgeni?"
"Ndio"
"Unatokea wapi?"
"Lusanga mkoani Tanga"
"Ndugu yako amekwambia anaishi sehemu gani?"
"Hapa hapa Dar"
"Dar ni kubwa broo, anaishi maeneo gani"
"Mnh, hilo sijui"
"Aai... kumbe we chizi. Unamtafuta mtu ambaye hujui anapoishi" yule kijana alimshangaa Ayubu na kumuacha amesimama bila ya kumpatia jibu la swali lake. Mara alifika msichana mmoja mrembo ambaye aliyasikia mazungumzo yale na kumsemesha Ayubu.
"Kwani kaka una tatizo gani?"
"Namtafuta ndugu yangu"
"Anaitwa nani?"
"Kondo"
"Yupoje?"
"Ni mrefu kidogo, maji yakunde halafu ana mwanya"
"Anhaaa! alikuwa anaishi Lusanga?"
"Enhee! Huyo huyo. si anapenda kuvaa suruali za jeans?"
"Ah! namjua"
"Naomba nielekeze basi anapoishi"
"Na mimi naenda hukohuko. Itakuwa vyema tukiongozana alisema yule dada na kumpokea Ayubu begi. Walisogea hadi karibu na geti la kutokea, yule dada akamfahamisha Ayubu kuwa mizigo ilikuwa ikisajiliwa kwenye kile kibanda, hivyo alimwambia amsubiri pale
Ayubu alisubiri kwa muda mrefu lakini yule dada hakutokea. Ikabidi amfuate pale getini. Lo! kumbe alikuwa amekwisha karibishwa jijini. Watu wakamfahamisha Ayubu kuwa alikuwa ameibiwa. Ayubu alinyanyua mikono na kuiweka kichwani. Alitoka nje na kuanza kuzurula mtaani asijue pa kuelekea.
******
Baada ya kutembea kwa muda mrefu pasipo kumuona mwenyeji wake Ayubu aliingia kwenye mgahawa kwa lengo la kupata chakula cha mchana kwasababu njaa ilikuwa ikimuuma sana. Aliagiza chakula na kuanza kula taratibum huku akiwaza namna ya kumpata rafiki yake Kondo. Baada ya kumaliza kula alifika dada mhudumu kudai malipo yake. Ayubu aliingiza mkono mfukoni na kujikuta hakuwa na hata senti. Lahaul! Kumbe alikuwa amekwishaibiwa pesa zote. Alimfahamisha dada muuza suala lile lakini yule dada akaonekana kuwa mgumu kuelewa.
“Samahani dada. Nimeibiwa”
“Unasemaje?”
“Nimepoteza pesa zangu”
“kwahiyo?”
“Sina hata senti”
“Baba nipe changu, usilete masihara na biashara”
“Kweli Aunt, nimeibiwa hela zote”
“Wewe kaka usinitanie. Nipe pesa yangu” alisema yule dada muuza na kumfanya Ayubu kuwa katika wakati mgumu. Wateja wengine nao waliungana na dada mwenye mgahawa na kumpa Ayubu jina la Tapeli. Walimzogoma na kumlazimisha alipe pesa ya watu vinginevyo wangemuitia kelele za mwizi apigwe hadi kupoteza uhai…..ITAENDELEA KESHO.
SIMULIZI YA KUSISIMUA
Taarifa za maisha bora na mazuri yaliyokuwepo JIJINI DAR ES SALAAM zilimvutia sana kijana AYUBU na kuingiwa na tamaa za kwenda kutafuta maisha jijini humo. Changamoto anazokumbana nazo zinamfanya amtafute muandishi Kizaro Mwakoba kwa msaada wa Kuandika Kitabu.

         >Soma Kuanzia Mwanzo>                          Soma Toleo Jipya hapa>>         

____________________________________________________________________________________
 
Top