Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, linawashilia watu wanne
waliojifanya kuwa askari polisi wakiwa na sare za jeshi hilo pamoja na
redio za mawasiliano ya upepo, ambazo zimekuwa zikiilingia mawimbi ya
mawasiliano yao.
Watu hao ambao majina yao yamehifadhiwa kwa sababu za kiupelelezi,
wamekutwa na pingu na wamekuwa wakitekeleza vitendo vya uhalifu kwa
kujifanya askari polisi.
Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Kamishna wa Polisi, Simon Sirro,
alisema watuhumiwa watatu waliwakamata Jumatano ya wiki iliyopita eneo
la Upanga karibu na Salender Bridge.
Alisema baada ya watu hao kuhojiwa, walikiri kufanya matukio ya ujambazi
wa kutumia silaha na kumtaja mwenzao anayeishi eneo la Kinyerezi jijini
hapa.
Alisema baada ya upekuzi nyumbani kwa mtuhumiwa huyo, walikuta sare
halisi za jeshi hilo zikiwemo za askari mwenye nyota tatu, simu ya upepo
na pingu.
Alisema uchunguzi umebaini watuhumiwa hao wamekuwa wakitumia sare hizo,
pingu na simu za upepo ili kufanya matukio ya uhalifu wakijifanya kuwa
ni polisi.
Alisema watuhumiwa hao wamekiri kufanya matukio mengine ya uhalifu
mikoani kwa kuweka vizuizi vya magogo barabarani na kuwapora wenye
magari.
“Tunawahoji mmoja mmoja tujue sare hizi, simu za upepo na pingu
wamezipata wapi maana ni za Jeshi letu," aisema Siro na kueleza zaidi,
"watu hawa wamekuwa wakiingilia mawasiliano yetu ya redio, wakati sisi
tunawasiliana na wao wanawasiliana.
“Usimwamini mtu anapokuja kwako na kusema yeye ni askari kisa amevaa
sare za polisi, lazima mjiridhishe ikiwezekana kudai kitambulisho.
"Wananchi watambue kuwa ndani ya jamii yetu kuna watu wa namna hii ambao
mwisho wao sio mzuri kwa sababu ipo siku wataacha familia zao.”
Wakati huo huo, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Kamishna wa Polisi, Simon Sirro, alisema wamekamata watuhumiwa wengine
watatu wa ujambazi wakiwa na bastola.
Alisema Februari 18 katika eneo la Kiwalani kwa Mkude walikamata
watuhumiwa hao wakiwa na bastola hiyo baada ya taarifa kutoka kwa raia
mwema ambaye alijulisha kuwa, watu hao majina polisi imeyahifadhi
walikuwa wanataka kufanya uhalifu.
Chanzo; Nipashe