WASHITAKIWA sita waliokuwa wanakabiliwa na makosa mawili ya kumiliki
vipande 53 vya meno ya tembo vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 149. 3
na uwindaji haramu kinyume na sheria wamehukumiwa kwenda jela miaka 120
na kulipa faini ya Sh bilioni 1.4 .
Waliokumbwa na adhabu hiyo ni Eliud Selema Mayunga (38) mkazi wa
kijiji cha Kiombo, Ramadhani Said maarufu “Biladuka” (47) mkazi wa
Itigi, na Leonard Oscar maarufu “Sunzu” (31) mkazi wa Karangari,
wilayani Manyoni.
Wengine ni Philemon Michael maarufu “Kanyonga” (31) mkazi wa Kitaraka
Itigi, Iddi Waziri au “Issah Ustadh” (30) mkazi wa kijiji cha Kiombo na
Jimmy Charles Lyimo (39) mfanyabiashara wa Tabora.
Mwanasheria wa Serikali, Petrida Mutta alidai mbele ya Hakimu
Mfawidhi Mwandamizi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, Joyce Minde
kuwa mnamo Machi 31 mwaka 2014 muda usiojulikana, washitakiwa
walikamatwa wakiwa na vipande hivyo nyumbani kwa Iddi Waziri.
Mutta aliiomba Mahakama itoe adhabu kali kutokana na vitendo vya uwindaji na biashara za nyara za serikali kuendelea kushamiri.
“Vitendo hivi haviwezi kufumbiwa macho kwa sababu vikifumbiwa macho, fahari ya nchi hii ya kuwa na wanyama pori itatoweka.”
Washtakiwa ambao wakili wao Josephat Raphael Wawa hakuwepo
mahakamani, kila mmoja kwa nafasi yake, aliiomba Mahakama impe adhabu
nafuu kutokana na kuwa kosa lao la kwanza.
Akitoa hukumu, Hakimu Minde alisema kuwa upande wa Jamhuri
umethibitisha bila kuacha shaka yoyote kwamba washtakiwa wanayo hatia
kwa makosa yote mawili. Alisema, kwa kosa la kwanza kila mmoja
atatumikia jela miaka 20 na kwa kosa la pili kila mmoja atalipa faini ya
Sh milioni 248. 8 tu.
Chanz:Habari Leo