Dereva wa Kampuni ya SYNOHYDRO inayojenga kwa kiwango cha lami barabara
ya kutoka Tunduru Mjini kwenda katika tarafa ya Nakapanya Wilayani humo
mkoani Ruvuma, amefariki dunia baada ya kusombwa na maji ya Mto
Muhuwesi.
Dereva huyo, Ally Ramadhani (31), alikumbwa na mkasa huo Alhamisi saa 11.30 jioni wakati akioga katika mto huo.
Taarifa zilizopatikana zilisema kuwa marehemu alikwenda kuoga katika mto
Muhuwesi baada ya muda wa kazi kwisha na kwamba aliteleza na kutumbukia
mtoni na kusombwa na mkondo mkali wa maji.
Taarifa hizo zilisema kuwa baada ya kuanguka, marehemu alisikika akiomba
msaada wa kuokolewa lakini kwakuwa wenzake walikuwa hawajui kuogelea
waliogopa kujitosa majini.
Mtu aliyekuwa na marehemu na ambaye aliomba jina lake lisitajwe
gazeitni, alisema dereva huyo alizama katika maji hayo na hakuonekana
tena.
Diwani wa kata ya Muhuwesi, Nurdini Mnolela, alithibitisha kuwepo kwa
tukio hilo na kwamba baada ya taarifa hizo kuwafikia, alianzisha msako
wa kuutafuta mwili wa marehemu kwa pamoja na watu waliojitolea wakiwa
wanafuata mto huo.
Mnolela aliendelea kufafanua kuwa, hata hivyo, kazi hiyo imekuwa ngumu
kutokana na wananchi wengi kutokuwa na ujuzi wa kupigambizi. Huenda
zoezi la kutafuta mwili likachukua muda mrefu, alisema.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Zubery Mombeji, alithibitisha tukio
hilo na kwamba ametuma kikosi kwenda kushirikiana na wananchi katika
msako huo.
Chanzo; Nipashe