Wakati wimbi la timua timua ya watendaji wazembe na waliotumia madaraka yao vibaya likiendelea, serikali ya Rais John Magufuli pia imewageukia ombaomba wa maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam, ambapo imeagiza ifanyike operesheni kabambe ya kuwaondoa.

Operesheni hiyo inatarajiwa kuanza wakati wowote kuanzia sasa na serikali imeagiza zoezi la kuwaondoa liwe limekamilika hadi kufikia Machi 10.

Ombaomba hao watasombwa hadi kwenye kambi ya JKT Ruvu, Pwani ambako watahifadhiwa kwa muda kabla ya maofisa wa Ustawi wa Jamii wa mikoa wanakotoka kuwachukua kwa mabasi ya kukodi.

Mmoja wa wafanyakazi wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ambaye hakutaka jina lake litajwe, aliliambia gazeti hili kuwa hivi sasa vikao vya kufanikisha mkakati huo vinaendelea katika Ofisi ya Waziri Mkuu.

Vikao hivyo ambavyo vimeshadumu kwa wiki moja sasa vinawahusisha maofisa wa Wizara ya Afya, Polisi, Magereza na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi). 

“Watakusanywa na kuhifadhiwa Ruvu JKT chini ya ulinzi mkali sana na kisha kurejeshwa kwao," alisema mtoa habari wetu ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini kwa sababu si msemaji.

"Kama mtu anatoka Dodoma (kwa mfano) basi maofisa Ustawi wa Jamii wa huko watahusika kumchukua na kumpeleka kwao na kama ni Morogoro basi wa Morogoro watahusika.” 

Mtumishi huyo ambaye ni mmoja wa wajumbe wa vikao hivyo, alisema ombaomba hao wamekuwa na kawaida ya kurudi jijini kila wanaporejeshwa makwao lakini operesheni ya safari hii itakuwa kali.

"Hakutakuwa na ujanja ujanja wa kurudi," alisema.
“Kwanza hawa watakaoondolewa watapewa onyo kali sana na zitawekwa sheria kali.

“Wakurugenzi wa Manispaa za Temeke, Ilala na Kinondoni wameambiwa kwamba iwapo omba omba hao wataonekana tena barabarani basi watawajibika wao… sasa sidhani kama kuna Mkurugenzi wa Manispaa ambaye atakubali kuwajibishwa.” 

Alipoulizwa kuhusu kuwepo kwa mkakati huo, Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Watoto katika Wizara ya Afya, Margaret Sawe alisema operesheni hiyo itakuwa kubwa na inatarajiwa kuanza kutekelezwa ndani ya wiki mbili kuanzia sasa.

Alisema hivi sasa wanaendelea kujipanga ili kuhakikisha mpango huo unafanyika kwa ustadi mkubwa ili usiharibu taswira ya serikali ya awamu ya tano.

Alisema operesheni hiyo kubwa na ya aina yake ni utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli kuhakikisha mji unakuwa katika hali ya usafi muda wote.

“Tumepanga wapelekwe kambi ya JKT Ruvu kama sehemu ya muda tu kabla ya kuwapandisha mabasi kwenda kwao," alisema Sawe na kueleza zaidi, "pale watakaa kwa muda na kutakuwa na huduma zote muhimu kama chakula na malazi.”

Alisema watakaokamatwa ni watoto wanaozurura barabarani wakiomba wapita njia pamoja na wazazi, ndugu na jamaa zao ambao hukaa pembeni ya barabara wakiwatuma kufanya kazi hiyo.

“Tumependekeza wakamatwe hata watu ambao huwapa fedha wale watu maana ndio wanasababisha waendelee kukaa barabarani.

"Kama una huruma kwanini usimchukue huyo mtu ukamwanzishie biashara au ukamwajiri kwenye kazi zako badala ya kumpa Sh.2,000 ambayo haitamsaidia kwa lolote?

“Unakuta mtu amewapanga ombaomba anawapa Sh.100 au Sh.200 sasa kiasi hicho kitawasaidia kuwaondoa kwenye umaskini au ndiyo unawaangamiza kabisa?

"Ndiyo maana tumeona tupendekeze wale wanaowapa nao wakamatwe na wafikishwe mahakamani.”

Alisema watu wanaowatumikisha watoto kuomba barabarani wana hela kwani hata wanapokamatwa na halmashauri husika na kufikishwa mahakamani hutozwa faini ya Sh.50,000 ambayo huilipa papo hapo na kuachiwa.

Alisema omba omba hao wamekuwa wakilipa hata kodi ya pango kwenye viambaza ambavyo wamekuwa wakilala usiku hivyo kuwaachisha kazi hiyo ni jambo gumu linalohitaji mkakati madhubuti.

“Wamekuwa wakikamatwa na kufikishwa mahakamani mara kadhaa na kule mahakamani Sheria inayotumika kuwahukumu ni ya uzururaji ambapo hutakiwa kulipa faini ya Sh.50,000… sasa wana kaumoja kao mwenzao akihukumiwa utashangaa wamechangishana na kumtoa na kesho anaendelea na shughuli hiyo,” alisema Sawe.

Desemba 4 mwaka jana, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki aliwaagiza wakurugenzi wa halmashauri za Jiji la Dar es Salaam, kuwaondoa ombaomba wote walioko katika barabara za jiji.

Alikuwa akizungumzia utekelezaji wa kauli ya Rais Magufuli ya kutumia siku ya Desemba 9 mwaka jana kufanya usafi ambao ungekwenda sambamba na kuondoa ombaomba hao, ambao wanachangia kuongeza uchafu.

Sadiki alisema viongozi wanawajibika kuhakikisha ombaomba hao hawarudi kwenye maeneo ambayo wataondolewa kwani imekuwa kawaida kwa wanaorudishwa makwao kurejea jijini.

Aprili mwaka 2014, Halmashauri ya Manispaa ya Temeke ilifanikiwa kuwakamata baadhi ya ombaomba walioonekana katika maeneo yake kwa lengo la kuwafikisha mahakamani na wengine kurejeshwa makwao.

Zoezi hilo liliendeshwa na maofisa wa Manispaa ya Temeke kwa kuzungunguka katika maeneo mbalimbali ya Manispaa hiyo kwa kushirikiana na askari wa Jiji.

Chanzo; Nipashe

HABARI NA MATUKIO ZAIDI YA KUSISIMUA BOFYA HAPA>>
 
Top