Muonekano wa jua litakavyokuwa wakati wa kupatwa kwa jua.
KESHOKUTWA Septemba 1, 2016 litatokea tukio kubwa la angani ambapo
kutakuwa na kupatwa kwa jua ambapo linatazamiwa kufanyika katika usawa
wa anga ya Tanzania.
Tukio hilo linatazamiwa kuanzia saa 4:17 asubuhi hadi 7:56 adhuhuri siku hiyo.
Mashabiki na wanataaluma wa anga kutoka duniani kote pamoja na
wanasayansi, wanafunzi pamoja na jamii ya Tanzania wataelekea Rujewa,
kusini mwa Tanzania, karibu na Mbeya, kushuhudia duara la Jua
linavyobadilika kuwa mithili ya pete.
Nchini kote Tanzania, siku hiyo mamilioni ya watu watashangaa kuona
Jua kali la utosini likimegwa kwa zaidi ya asilimia 90 kwa kufunikwa na
mwezi katika tukio hilo la kupatwa kwa jua. Hali hiyo italiacha jua
lionekane kama pete au hilali nyembamba au mithili ya mwezi mwandamo.
Watu wanaoishi ndani ya ukanda wenye upana wa kilometa 100
unaokatisha kusini mwa Tanzania, kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
kuelekea Katavi, Mbeya, Ruvuma hadi Masasi na kuingia Msumbiji, siku
hiyo wataona jua kama duara jembamba mithili ya pete, kwa vile asilimia
98 ya jua katika maeneo yao litakuwa limejificha nyuma ya mwezi. Kupatwa
huko kwa jua kunaweza kuonekana kwa usalama na watazamaji, lakini
inabidi kutumia vichuja maalum vya mwanga wa jua.
Tukio la kupatwa kwa jua ni la kusisimua na la nadra sana kutokea
katika maisha ya mtu na baadhi ya dini kama Uislamu zinawataka watu
wakati wa kipindi hicho kuwa kwenye swala maalumu. Vijana wengi katika
kizazi hiki kipya watakuwa hawajaona tukio hili na hivyo ni tukio
litakalowasisimua na wanafunzi ambao wamekuwa wakijifunza mashuleni
watapata ushahidi wa moja kwa moia siku hiyo.
Wengine watazidi kujifunza sayansi ili kuelewa kwa nini kinatokea
kile wanachokiona. Kwa hiyo tukio hili linaweza kutumiwa na shule na
taasisi za elimu kuendeleza sayansi na kuvuta wanafunzi kujiendeleza
kisayansi na hasa kuelewa mizunguko mbalimbali iliyopo katika mfumo wetu
wa sayari pamoja na anga za juu kwa ujumla. Bila shaka wataongeza
uelewa wa sayansi na umuhimu katika kuelewa maumbile ya ulimwengu wetu.
Kupatwa huku kwa jua kutatokea siku ya Alhamisi ambapo wanafunzi
wengi watakuwa shuleni na litatokea wakati wa masomo. Kwa vile mchakato
wote utaendelea kwa masaa manne hivi, kati ya saa 4:00 asubuhi hadi saa
8:00 mchana wanafunzi wataweza kushirikiana kuangalia, kusimulia na
kujadili tukio ili kulielewa vizuri na kuandika ripoti madarasani mwao.
Tukio jingine kubwa la kupatwa kwa Jua kama hili halitatokea miaka 15
ijayo, kwa hiyo tunahitaji kutumia fursa hii kwa ukamilifu kujifunza.
Ili kuangalia kupatwa huko, kila mmoja atahitaji kutumia kikinga
macho kinachochuja mwanga wa Jua kiitwacho Kitazamia Jua. Nini hatari
kuangalia jua lililopatwa kwa macho moja kwa moja au hata kutumia
vichujio vingine vya kiza vilivyotengenezwa mitaani. Kitazamia Jua
maalumu ni kifaa rahisi kilichotengenezwa kutokana na kichuja nguvu ya
jua ambacho kinaondoa mionzi haribifu kwa asilimia 99.999.
Miwani hiyo maalumu ya Jua inaweza kutengenezwa Tanzania kwa gharama
isiyozidi Sh 500 kila moja, ikiwemo kuchapa fremu za kadbodi na kichuja
nguvu ya jua (polymer filter) kinachoagizwa kutoka Marekani.