Rais John Magufuli, ameponda Mkataba wa Serikali na Kampuni ya kufua umeme ya IPTL, akisema wakati umefika nchi iachane na umeme wa wafanyabiashara na iwe na wake yenyewe.
Akiweka jiwe la msingi kwenye mitambo ya kufua umeme ya Kinyerezi II, Rais Magufuli alisema: “Ni lazima nchi yetu tuachane na umeme usio na uhakika, umeme wa kukodishakodisha, umeme wa kutumia watu na ndiyo maana kumekuwa na matatizo mengi mara IPTL, mara nini, ni kwa sababu tulizoea maumeme ya kukodisha kodisha, ya wafanyabiashara, kwa hiyo hatua hii ya umeme wetu, ambao tutaumiliki sisi wenyewe tutafanikiwa katika maendeleo.
“Tuachane na  mitambo ya kukodi, tumechoka kufanyishwa biashara na wawekezaji, tunalipia `capacity charge' za ajabu ajabu halafu tunalipia bei ya ajabu.
“Tunawapa shida Watanzania wa hali ya chini, kila mmoja anahitaji umeme, lakini wengine wanashindwa kuuvuta  kwa sababu umeme ni wa juu.”
Katika kashfa ya Tegeta Escrow iliyosababisha kutafunwa kwa takribani Sh. bilioni 300, mbali na kung’oa baadhi ya mawaziri na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, baadhi ya maazimio yaliyopitishwa na Bunge mpaka leo hakuna kilichofanyika.
Azimio la saba la Bunge lilisema kwa kuwa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imeonyesha kuwa, Tanesco imekuwa ikitumia mabilioni ya fedha kulipa gharama za umeme unaozalishwa na IPTL na hivyo kuathiri hali ya kifedha ya shirika hilo, serikali iangalie uwezekano wa kununua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na kuimilikisha kwa shirika la umeme nchini kwa lengo la kuokoa fedha.
Agizo hilo lililotolewa mwishoni mwa mwaka 2014, lakini mpaka leo halijatekelezwa na inadaiwa kuwa kila mwezi Tanesco inailipa IPTL Sh. bilioni nane, izalishe ama isizalishe umeme.
Hivi karibuni, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali iliyowasilisha ripoti yake Bunge la 10 juu ya Escrow, alisema: “Mapato ya nchi makubwa kuliko ya utumbuaji majipu yanaendelea kupotea. Mkataba wa IPTL bado unaendelea kunyonya nchi na serikali inatazama Sh. bilioni nane zinalipwa IPTL na PAP kila mwezi. Katika siku 100 tangu Rais Magufuli aingie madarakani, jumla ya Sh. bilioni 30 zimeshalipwa kwa IPTL/PAP.”
UMEME MUHIMU
Rais Magufuli alisema umeme ni kichocheo muhimu katika ukuaji wa uchumi popote duniani na kwamba matumizi ya nishati hutumika kama kipimo cha maendeleo ya nchi husika.
“Hutumika kuongeza ufanisi katika shughuli za uchumi na kuboresha huduma za kijamii kama elimu afya.. bila ya umeme wa uhakika ndoto ya uchumi wa viwanda haitatimia, tutakapokuwa na umeme maana yake ndoto ya kujenga viwanda vidogo, vya kati na vikubwa itafanikiwa na vitatengeneza ajira,” alisema.
Rais alisema kwa mujibu wa takwimu zilizopo, uwezo wa nchi wa kuzalisha umeme ni takriban megawati 1,200 kwa mwaka.
“Taarifa za waziri leo tumefikia megawati 1,026, hivyo kila Mtanzania anatumia voti 30 kwa mwaka, ikilinganishwa na nchi zilizotuzunguka mfano Kenya kila Mkenya anatumia voti 40 kwa mwaka, China voti 490 kwa mwaka, Afrika Kusini voti 500 kwa mwaka, Marekani kila Mmarekani anatumia voti 1,683 kwa mwaka, kwa hiyo sisi bado tupo chini,” alisema.
Rais Magufuli alisema kwa kutambua hilo, wakati wa kampeni za uchaguzi zilizofanyika mwaka jana  walizungumzia kuhusu adhma ya nchi iwe ya viwanda, lakini walitambua hawawezi kufanya hivyo bila kuimarisha umeme.
“Leo nimefarijika kuona katika kipindi cha miezi mitatu na ushee nikiwa madarakani nimealikwa kuweka jiwe la msingi la mradi wa Kinyerezi II utakaotoa megawat 240, hii ni hatua nzuri.
“Ninafahamu mradi huu ulikwama siku nyingi, serikali ya Japan iliamua kutupa Dola zinazokadiriwa kufika milioni 300, lakini sharti lao kubwa tuchangia asilimia 15 (Dola milioni 120) na Japan Dola milioni 292 . Tumekaa zaidi ya miaka miwili tukiwa tumeshindwa kuzipata asilimia ya dola hizi ili tupate zao,” alisema. 
Aliongeza kuwa aada ya kuimarika kwa makusanyo Novemba na Desemba, mwaka jana, walitoa maelekezo zikapatikana fedha hizo, ndipo wajapani nao walipotoa Dola 292.
TANESCO NA WIZARA
Rais Magufuli alisema pamoja na kwamba yeye ni mgumu kupongeza, lakini kwa jitihada zilizofanyika wamekwenda kwenye mwelekeo.
“Tanzania ni tajiri, tuna gesi ya kutosha kwa taarifa zilizopo tuna futi za ujazo zaidi ya trilioni 57, kwa hiyo kila mahali kuna gesi hata hapa Ruvu kwa watani zangu, nako kuna gesi wanalima mpunga juu, lakini ndani kuna gesi,  haiwezekani nchi tajiri yenye gesi kila mahali tunalalamika masuala ya umeme, tukiwa na umeme wa kutosha hata gharama zitashuka,” alisema.
Aliongeza: “Kila moja atawasha kwa umeme, hayo ndiyo maisha tunayoyatafuta Watanzania, Mungu ametupa kila kitu hapa, zipo nchi Ulaya zinasafirisha gesi kutoka Urusi  sisi ipo hapa hapa, haiwezekani tukaendelea kuwa maskini, lakini na wasomi wapo, iweje tuwe maskini,” alihoji.
Alisema amepata taarifa mradi wa Kinyerezi I wataongeza megawati 185 na kandarasi anahitaji Dola milioni 20.
“Sasa kama tumetoa milioni 120 (dola) kwa nini tushindwe hizi Dola milioni 20, mwambie mkandarasi tutazitafuta hata mwezi huu zitapatikana ili aanze, tunataka umeme uwe kila mahali kwa sababu vyanzo vipo mambo ya kutumia vyanzo vya umeme vya maji yawezekana wakati wake umepita,” alisisitiza. 
Aliongeza: “Tanzania ina kila kitu hata uranium inaweza kutumika kama chanzo cha umeme, tuna makaa ya mawe, gesi maji lakini tunalalamika  hakuna umeme na wasomi tumewasomesha, sijui wanaenda kujifunza nini huko , ndio maana nasema wizara mmenifuraisha, nendeni kwa speed kubwa zaidi,”alisema.
Alisema ndio maana akasema hachagui mwanasiasa bali mchapakazi kwa sababu  maendeleo hayana chama.
“Uwe CUF , Chadema au usiwe na chama wote mnahitaji umeme, ndio maana nikachagua watu wa kuchapa kazi bila kubagua vyama zao, nawahakikisha Watanzani serikali yangu itafanya kazi kweli kweli, mlituchagua bure hatujawahonga, lazima tuwafanyie kazi ili tuondoe kero, tunawahakikisha bila kigugumizi tumejipanga kufanya kazi, atakayetukwamisha atakwama yeye na kuondoka ataondoka yeye siku hiyo hiyo,” alisema.
Alisema Watanzania wamechoka kusubiri kutoka uhuru haiwezekani waendelee kuwa maskini  wakati nchi imebarikiwa na kuwa na rasilimali kama Tanzanite, bahari,  maji , maziwa, dhahabu, almasi  na makaa ya mawe.
 “Lazima tutumie nguvu zetu zote, kama tatizo lipo ndani ya serikali, niachieni mimi nitawanyoosha waliopo ndani ya serikali na ninyi wananchi isaidieni serikali kwenda mbele wale wanaotaka kutuchelewesha kwa ajili ya kazi muwapuuze, kila mmoja ajipange kufanya kazi,” alisema.
KUHUSU FIDIA
Alisema anafahamu wapo waliolipwa fidia Sh. bilioni 30 na wachache ambao hawajalipwa kama Sh. bilioni mbili.
“Tutawaletea hizi fedha mlipwe, lakini wale waliolipwa wasifanye ujanja ili walipwe tena. Hakuna fedha za bure lazima niwaeleze ukweli hili siyo shamba la kufanya biashara, tutazileta fedha hizi wapo wawili walikataa kuzipokea shauri yao, lakini wakitaka kuzipokea waje kuchukua, wakiona wanataka kwenda mahakamani waende, wale wanaostahili tutawalipa,” alisema.
Aidha, alimshukuru Balozi wa Japan na Mtendaji Tanesco na kueleza kuwa mradi upo Kinyerezi kuna vijana na kina mama na wazee wapewe nafasi ya kwanza kupata ajira hapo.
“Ombi langu vijana mkipata nafasi msiibe vifaa vitakavyotumika hapa, mjue huu ni mradi wa Watanzania ni wetu sote, tunataka ukamilike mapema, unapoiba vifaa au mafuta, ujue wewe ni chanzo cha kuchelewesha maendeleo, mtangulizeni Mungu mbele, ulipwe fedha ili baadaye mradi uwanufaishe wote,” alisema.
Alisisitiza kuwa maendeleo yataletwa na Watanzania wote kwa kuwaeleza wana Kinyerezi kuwa anafahamu wana matatizo ya maji, lakini baada ya umeme kupatikana ndiyo mwanzo mzuri wa kupata maji.
 
Top