
Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela
akiwaonesha wandishi wa habari ujumbe ulioachwa na marehemu Emmanuel Moshi
baada ya kumuua mfanyabiashara mwenzake Didas Alphonce kwa kumkata na
shoka kichwani na kisha yeye kujiua kwa kujinyonga. Picha Joyce Joliga
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kudai uchunguzi wa awali unaonyesha
wafanyabiashara hao walikuwa wanadaiana pesa.
Songea. Mfanyabiashara wa mbao Manispaa ya Songea, Emmanuel
Moshi (40), mkazi wa Marangu, mkoani Kilimanjaro amemuua mfanyabiashara
mwenzake aliyetambuliwa kwa jina la Didas Alphonce (64), mkazi wa Kilema
Kilimanjaro kwa kumpasua kichwa kwa shoka, kisha yeye mwenyewe kujinyonga kwa
kutumia kamba ya katani katika stoo ya nyumba waliyokuwa wakiishi.
Inadaiwa kuwa Moshi alichukua uamuzi huo baada ya Alphonce kumdhulumu zaidi
ya Sh87.4 milioni.
Wakizungumza na gazeti hili jana, watu wa karibu na wafanyabiashara hao
ambao hawakupenda majina yao kuandikwa kwenye gazeti, walidai kuwa
wafanyabiashara hao walikuwa wakiishi nyumba ya ndugu yake, Didas na kufanya
biashara za kuuza mbao pamoja.
Walidai kuwa, Desemba 30 mwaka jana, wafanyabiashara hao walikuwa wakinywa
pombe kwenye Bwalo la Magereza na Moshi alikuwa akilalamika kudhulumiwa na
Didas.
Mashuhuda hao waliongeza kuwa tangu siku hiyo, wafanyabiashara hao
hawakuonekana tena hadi jana.
Ilidaiwa kuwa, mwenye nyumba huyo alitumia funguo zake za akiba kufungua
nyumba hiyo na kukuta mwili wa mjomba wake ukiwa umepigwa na shoka na tayari
umeanza kuharibika.
Mtu mmoja ambaye jina lake tunalihifadhi alitoa taarifa kituo cha polisi na
walipofika waliubaini pia mwili wa Moshi aliyejinyonga.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela alithibitisha kutokea kwa
tukio hilo na kudai uchunguzi wa awali unaonyesha wafanyabiashara hao walikuwa
wanadaiana pesa.
Alisema Mosha ameacha ujumbe mrefu wa karatasi nne aliouandika kuhusiana na
mauaji hayo.
Ujumbe huo: “Kataeni wadhulumaji kati ya matajiri na maskini, nimeondoa
dhambi kubwa ya dhuluma iliyokuwa ikinitesa ulimwenguni, wadhulumaji
wasifumbiwe macho jamii iniunge mkono kuondoa watu hawa. “Dhuluma aliyonifanyia
mtu huyu imekatisha maisha yangu.”
Chanzo: Mwananchi