WIZARA ya Elimu, Sayansi na Ufundi imetoa waraka wa elimu kuhusu elimumsingi bila malipo na kutoa orodha ya shule za msingi 11 za Serikali ambazo hazihusiki na utoaji wa elimu bure uliotangazwa na Rais John Magufuli. Elimumsingi inajumuisha elimu ya awali, ya msingi na sekondari ambayo itaanza Januari mwakani.
Katika Waraka Elimu Namba 6 wa Mwaka 2015 kuhusu utekelezaji wa elimu bure kwa shule za msingi na sekondari, wizara hiyo imetaja shule hizo kuwa ni Shule ya Msingi Olympio (Dar es Salaam); Shule ya Msingi Diamond (Dar es Salaam); Shule ya Msingi Oysterbay (Dar es Salaam); Shule ya Msingi Iringa (Iringa) na Shule ya Msingi Mkapa (Mbeya).
Nyingine ni Shule ya Msingi Angaza (Mbeya); Shule ya Msingi Nuru (Mbeya); Shule ya Msingi Lupilisi (Ruvuma); Shule ya Msingi Tanga (Tanga); Shule ya Msingi Arusha (Arusha) na Shule ya Msingi Kisimani iliyoko mkoani Arusha.
Wizara hiyo pia imesema waraka huo hauzihusu shule zinazomilikiwa na mashirika ya umma ama taasisi za umma ambazo zinaendeshwa kwa taratibu sawa na shule za binafsi. Katika waraka huo, wizara hiyo imetoa majukumu yanayotakiwa kufanywa na Wizara hiyo, Tamisemi, wakurugenzi wa manispaa na halmashauri ya wilaya, wakuu wa shule, bodi za shule, wazazi na wananchi.
Majukumu ya wazazi na walezi Kuanzia Januari, wazazi wanatakiwa tu kununua sare za shule na michezo, vifaa vya kujifunzia vikiwemo madaftari na kalamu, na chakula kwa wanafunzi wa kutwa na kugharimia matibabu kwa watoto wao.
Wanatakiwa pia kulipia nauli ya kwenda shule na kurudi kwa wanafunzi wa kutwa na wanafunzi wa bweni wakati wa likizo; kununua magodoro, shuka, vifaa vya usafi binafsi kwa wanafunzi wanaosoma shule za bweni na wanaoishi katika hosteli zinazotumiwa na serikali; na kukemea na kutoa taarifa kuhusu mienendo inayokwenda kinyume na elimumsingi bila malipo.
Chanzo: HABARI LEO