WANANCHI wa vijiji vya Kahe-Useri na Ngaseni kata ya Ubetu Kahe
wilayani Rombo, mkoani Kilimanjaro wamekataa taarifa za mradi wa umeme
vijijini (REA), unaotekelezwa na kampuni ya Spencon ya Dar es Salaam kwa
madai unafanyika kwa ubaguzi na misingi ya rushwa.
Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa mkoa huo, Amos Makalla ameagiza
kufanyika kwa kikao cha utambulisho kitakachohusisha wafanyakazi wa
Shirika la Umeme nchini(Tanesco) wilaya ya Rombo ili kuwatambua
watumishi waliokuwa wakichukua Sh 30,00 kama rushwa kwa wananchi, ikiwa
ni sharti la kufungiwa umeme.
Katika mikutano ya hadhara iliyofanyika katika vijiji hivyo, Mkuu wa
mkoa alikuwa na lengo la kukagua utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi
wa umeme vijijini pamoja na kukabili changamoto zinazojitokeza.
“Wote mmesikia mkandarasi na Tanesco katika wilaya hii mnalalamikiwa
kuchukua Sh 30,000 kwa zaidi ya watu 44 wanaohitaji umeme, nataka
Jumatatu (leo) mfanye utambulisho kwa wafanyakazi ili wananchi
wawabainishe wanaochukua rushwa,”alisema.
Alimtaka mkuu wa wilaya hiyo, Lembris Kipuyo kuongoza utambulisho huo
ili kuhakikisha wananchi hawanyanyaswi kwa misingi ya rushwa, jambo
linalochangia kuichukia serikali yao. Makalla alihoji kama gharama za
fomu ya maombi ya kuunganishiwa umeme ni Sh 5,900 kwa nini wafanyakazi
hao wawatoze wananchi kiasi kikubwa cha fedha ambacho kinaweka daraja
baina ya masikini na tajiri.
Mkuu wa mkoa alikuwa akizungumzia hoja za baadhi ya wananchi, Richard
Uiso na Merina Shirima waliodai mradi huo wa umeme umeelekezwa kwa watu
wenye uwezo kiuchumi, licha ya kwamba walistahili kupata wao ambao wapo
katika njia kuu zilizoainishwa katika mradi huo.
“Mkuu wa mkoa huyu mkandarasi na hawa wafanyakazi wa Tanesco wanasema
uongo lakini wamepeleka umeme kwa matajiri licha ya kwamba walitutoza
Sh 30,000,” alisema. Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Rombo, Joseph
Selasini alisema alipewa malalamiko kwamba mkandarasi kampuni ya Spencon
amebadili njia ya kupitisha umeme na kuwafungia wateja 167 ambao
asilimia kubwa wamepewa kwa misingi ya rushwa.
“Hao wote wanaotajwa kufungiwa umeme ni wale wenye uwezo na hawakuwa
katika mradi...huyu mkandarasi amechepusha mradi kufuata matajiri, ili
kuepusha yote haya atuoneshe makisio ya tathmini ya mradi (BOQ) tutazame
njia zilizotajwa katika mradi,” alisema.
Akijibu tuhuma za rushwa, Kaimu Meneja wa Tanesco mkoani hapa,
Fataely Maro alisema wanatekeleza mradi kwa mujibu wa sheria na siyo
vinginevyo. Naye msimamizi wa mradi huo kutoka kampuni ya Spencon,
Bumarwa Mushumbuzi alisema katika kijiji cha Kahe amejenga umeme wa
msongo mkuu kwa umbali wa Km 3.1 na amefunga Transfoma yenye uwezo wa
KVA 100.
Kazi nyingine ni kufunga mtandao mdogo wa umeme kwenda kwa wateja Km
3.8, umeme mdogo kwa ajili ya mashine Km moja na kufunga mita kwa wateja
167, taarifa ambayo ilipingwa na wananchi hao.
Chanzo: HabariLeo