MTOTO mchanga ameibwa katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Felix Ntibenda ameagiza vyombo vya ulinzi na
usalama kusaka watu walioiba mtoto huyo mwenye umri wa siku tatu.
Alisema wizi huo ulifanyika Machi 15 mwaka huu, baada ya mkazi wa
Kijiji cha Sukuro, Kata ya Komolo wilayani Simanjaro, Sinyati Lucas(25)
kufika naye hospitalini hapo baada ya kujifungulia nyumbani.
Mkuu wa mkoa alisema mama huyo baada ya kujifungua akiwa nyumbani,
kondo la nyuma lilishindikana kutoka ndipo alikimbizwa Hospitali ya
Mount Meru.
Ntibenda, alisema taarifa zinasema mama huyo alitokwa na damu nyingi
na kupoteza fahamu hivyo ndugu zake kulazimika kuchukua gari la wagonjwa
hadi Mount Meru.
Alisema alifika hospitalini akiwa ameongozana na mumewe, Lucas
Ngaraha, mama mkwe, Natamwaki Ngaraha na mkunga aliyemzalisha, Maria
Nengweikai.
Mkuu huyo wa mkoa ameagiza polisi kuwahoji wauguzi wa zamu, walinzi
wa kampuni ya ulinzi inayolinda hospitali hiyo, mama mkwe na mwanamke
mmoja ambaye aliletwa na mumewe ambaye hakutajwa jina.
Alisema wauguzi walimruhusu mzazi huyo kulala na wasaidizi wawili
akiwemo mama mkwe na mwanamke aliyeletwa na mumewe kutokana na ukaribu
waliokuwa nao.
Hata hivyo, kwa mujibu wa mkuu wa mkoa, mzazi haruhusiwi kukaa na
wasaidizi wodini lakini katika tukio hilo waliruhusiwa wanawake wawili
wodini kwa kisingizio cha kumsaidia mzazi.
Alisema polisi imeshaanza kuhoji baadhi ya watu kuhusu tukio hilo.
Ntibenda alisema baada ya uchunguzi kukamilika wahusika watafikishwa
kwenye vyombo vya sheria.