SIKU moja baada ya baadhi ya Kamati za Kudumu za Bunge kuhusishwa na
tuhuma ya kashfa ya rushwa, Spika wa Bunge, Job Ndugai amefanya
mabadiliko ya baadhi ya wajumbe wa kamati hizo ili kuzingatia mahitaji
mapya na changamoto zilizojitokeza baada ya kuunda Kamati hizo Januari
mwaka huu.
Mabadiliko hayo yamegusa takribani wenyeviti na makamu wenyeviti wote
wanaotuhumiwa kuhusika kwa namna moja ama nyingine na vitendo vya
rushwa kama ilivyoripotiwa na moja ya gazeti la kila siku (si
HabariLeo).
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kitengo
cha Mawasiliano cha Bunge, mabadiliko hayo yamefanywa chini ya kifungu
cha 116(3) cha Kanuni za Kudumu za Bunge kinachompatia Spika Mamlaka ya
kuteua wabunge na kuunda Kamati mbalimbali za Bunge.
Katika taarifa hiyo, imebainisha kuwa mabadiliko hayo yaliyowagusa
pia wenyeviti, makamu mwenyekiti au wote wawili, yatalazimisha kamati
hizo zilizoathirika na mabadiliko hayo kufanya uchaguzi wa viongozi kwa
mujibu wa kanuni ya 116 (10).
Alitaja kamati zilizoathirika na mabadiliko hayo zitakazohitaji ama
mwenyekiti na makamu mwnyekiti au wote kuwa ni Kamati ya Ardhi,
Maliasili na Utalii, Kamati ya Nishati na Madini, Kamati ya Uwekezaji wa
Mitaji ya Umma na Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na
Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.
Ndugai alitaja wabunge waliobadilishiwa kamati kuwa ni aliyekuwa
Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira Dk Mary Mwanjelwa
anayekwenda katika Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira na aliyekuwa
Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Martha Mlata anayekwenda
Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala.
Wengine ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uwekezaji na Mitaji
(PIC), Richard Ndassa na aliyekuwa mjumbe wa Kamati ya PIC, Selemani
Zedi ambao wote wamehamishiwa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala.
Aidha, Ndugai alitaja wajumbe wengine wa Kamati kuwa ni aliyekuwa
Mjumbe wa Kamati ya LAAC, Victor Mwambalaswa, aliyekuwa Makamu
Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Dk Raphael Chegeni
na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya LAAC, Kangi Lugola ambao wote
wanahamishiwa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.
Wabunge wengine waliohamishwa ni aliyekuwa Mjumbe wa Kamati ya Huduma
na Maendeleo ya Jamii Margaret Sitta anayekwenda Kamati ya Utawala na
Serikali za Mitaa, Mjumbe wa Kamati ya Viwanda, Abdulaziz Abood
anayekwenda LAAC na Mjumbe wa Kamati ya Viwanda, Suleiman Nchambi
anayehamia Kamati ya Katiba.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Ndugai pia aliwahamisha aliyekuwa Mjumbe
wa Kamati ya Viwanda Ibrahim Raza anayekwenda Utawala, Sylvestry Koka
aliyekuwa Kamati ya Mambo ya Nje na kuhamishiwa Viwanda na Peter
Lijualikali aliyekuwa Utawala na kuhamia Kamati ya Huduma za Jamii.
Wabunge wengine ni Profesa Anna Tibaijuka aliyekuwa Kamati ya Sheria
Ndogo anayehamishiwa Kamati ya Miundombinu, Dunstan Kitandula aliyekuwa
Kamati ya Mambo ya Nje, Ezekiel Maige aliyekuwa Kamati ya Hesabu za
Serikali (PAC), Innocent Bashungwa aliyekuwa Bajeti ambao wote
wanahamishiwa Nishati na Madini.
Aidha, katika mabadiliko hayo, wabunge wawili ambao ni Azza Hamad na
Zaynab Vullu waliokuwa Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa
wamehamishiwa Kamati ya Ukimwi. Wengine ni Shally Raymond aliyekuwa
Mambo ya Nje sasa anakwenda PAC, Joseph Selasini aliyekuwa Mambo ya Nje
sasa amehamishiwa LAAC, Emmanuel Mwakasaka aliyekuwa LAAC, amehamishiwa
Miundombinu na Suleiman Sadick aliyekuwa LAAC amehamishiwa Kamati ya
Huduma za Jamii.
Katika mabadiliko hayo, pia wabunge wengine ambao ni Sixtus Mapunda
aliyekuwa Ardhi amehamishiwa Ukimwi, Hamoud Jumaa aliyekuwa Kamati ya
Ardhi naye amehamishiwa Utawala na Serikali za Mitaa, Wilfred Lwakatare
aliyekuwa Ardhi sasa yupo Nishati na Boniphace Getere aliyekuwa Ardhi
amehamishiwa Huduma za Jamii.
Wakati Spika akifanya mabadiliko hayo, baadhi ya wenyeviti na makamu
wenyeviti wa kamati hizo zilizofanyiwa mabadiliko walituhumiwa kuhusika
katika kashfa ya kuomba na kupokea rushwa kwa mujibu wa moja ya gazeti
linalotoka kila siku (si HabariLeo), ingawa wahusika wote walikanusha
tuhuma hizo.
Wenyeviti wanaotuhumiwa kuhusika na kashfa hiyo ni Mbunge wa Sumve,
Ndassa, Mbunge wa Busega, Dk Chegeni, Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola,
Mbunge wa Sumbawanga Aeshi na wabunge wa Viti Maalum Mlata na Dk
Mwajelwa.