Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu
KARANI wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na
Teknolojia (IMTU), Bakari Mlanga (23) amehukumiwa miaka 27 jela huku
Ahmed Mbinjika (25) atatumikia kifungo cha miaka 12 baada ya kupatikana
na hatia ya kughushi fomu za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
Washtakiwa hao walihukumiwa kifungo hicho jana katika Mahakama ya
Wilaya ya Ilala na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Juma Hassan. Hakimu Hassan
alisema upande wa mashitaka, ulileta mashahidi watano kuthibitisha
mashitaka hayo na kwamba Mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa
mahakamani hapo.
Alisema kuwa mshtakiwa Mlanga amekutwa na hatia katika makosa tisa,
ambapo kwa kila kosa kwa makosa manane, atatumikia miaka mitatu na kosa
la tisa kutumikia kifungo cha miezi 12. Pia alisema Mbinjika amekutwa na
hatia kwa makosa manne, ambayo kila kosa atatakiwa kutumikia kifungo
cha miaka mitatu.
Alisema kupitia mashahidi, washtakiwa walighushi fomu hizo kuchukulia
dawa za kisukari na shinikizo la damu katika maduka mbalimbali yaliyopo
jijini Dar es Salaam. Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, Wakili wa
Serikali, Florida Wenslaus aliiomba Mahakama kutoa adhabu kwa mujibu wa
sheria, iwe fundisho kwao na wengine wenye tabia kama hizo.
Katika mashitaka yao, ilidaiwa kuwa Desemba 15, 2014 washtakiwa
walighushi fomu ya NHIF ya Tito Mfilinge, kuonesha kuwa imesainiwa na Dk
Emma Chambenga kuonesha kwamba ni halali kutumika.
Pia ilidaiwa katika tarehe hiyo hiyo, walighushi fomu ya NHIF ya
kuchukulia dawa ya Felister Msendekwa iliyoandikwa Desemba 9, 2014 na
kuonesha kuwa ilisainiwa na daktari huyo na walifanya makosa hayo mara
nyingi kwa nyakati tofauti.