Mbeya. Samaki wanaoingizwa nchini wakitokea nchi jirani wanadaiwa kusababisha madhara ya kiafya ikiwamo wanaume kuota matiti na wanawake kuota ndevu.
Samaki hao huingizwa nchini kupitia mipaka ya Kasumulu-Kyela na Malawi na ule wa Tunduma na Zambia.
Kutokana na uwapo wa taarifa za samaki hao, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla ameagiza mamlaka zote zinazohusika na usimamizi na ulinzi mipakani kuongeza nguvu ya udhibiti na uhakiki wa bidhaa zote zinazoingizwa nchini.
“Mbeya na Songwe ni kitovu cha biashara ya samaki wanaotoka nje ya nchi. Lakini kibaya zaidi kuna taarifa za uwapo wa samaki kutoka nje wanaodaiwa kuhatarisha afya za watu. Nimesikia kina baba wakiwala huota matiti na wanawake huota ndevu kwa wingi na athari zingine nyingi,” alidai Makalla na kuongeza:
“Sipingi kuingizwa kwa vyakula kutoka nje ya nchi, lakini ni vizuri utaratibu ukafuatwa, idara zote mipakani zijiridhishe na bidhaa zote zinazoingizwa hapa kwetu.”
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Uvuvi nchini, Magese Bulayi alisema mikoa ya Songwe na Mbeya ni kitovu cha biashara ya mazao ya majini.
Alitoa wito kwa wafanyabiashara wa samaki kuzingatia maagizo na maelekezo yatolewayo na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) pindi waingizapo samaki hao kupitia mipaka ya Tunduma na Kasumulu wilayani Kyela.
Bulayi alisema samaki hao wana madahara kwa binadamu na Idara ya Uvuvi makao makuu baada ya kupata taarifa, tayari imewatuma maofisa wake kutoa elimu kwa wadau kuhusu utaratibu wa uingizaji wa biashara ya vyakula vitokanavyo na mazao ya majini.
Mmoja wa wafanyabiashara wa samaki katika Soko la Soweto jijini Mbeya ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema samaki wanaowaagiza huletewa wakiwa wamefungwa na juu huandikwa samaki aina ya sato, migebuka, kibua, au magege.Hivyo hawawezi kujua kama wana madhara kwa binadamu. “Ila siku za hivi karibuni tunapokea malalamiko mengi kutoka kwa wateja wetu wanaodai kuwa tunawauzia samaki waliooza,” alisema.
Mkazi wa Ruanda jijini hapa, Atuganile Kasyupa alisema kwa sasa samaki anaonunua hawana radha.
“Tukiwauliza wauzaji wanasema eti kwa sababu ya balafu,” alidai Kasyupa.
MATUKIO ZAIDI YA KUSISIMUA BOFYA HAPA>>
MATUKIO ZAIDI YA KUSISIMUA BOFYA HAPA>>