WATU watatu wamekufa papo hapo na wengine wanane kujeruhiwa baada ya
basi lenye namba za usajili T 402 CRY aina ya Scania mali ya Kampuni ya
Kisbo – Safari kupinduka mkoani Morogoro. Basi hilo lilikuwa likitoka
mkoani Tabora kwenda Dar es Salaam.
Imeelezwa kuwa basi hilo lilipinduka wakati likijaribu kukwepa gari
lingine eneo la Kwambe, wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro kwenye
barabara kuu ya Dodoma – Morogoro.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Leonce Rwegasira alisema
kuwa tukio hilo lilitokea majira ya saa 12: 30 jioni, juzi, mwaka huu
eneo la Kwambe, kata ya Dumila, tarafa ya Magole wilayani Kilosa mkoani
Morogoro kwenye barabara kuu ya Dodoma- Morogoro.
Alisema basi hilo likiendeshwa na Davis Samora (38) mkazi wa Dar es
Salaam liliacha njia na kupinduka wakati likijaribu kukwepa gari lenye
namba za usajili T957 BUV aina ya Scania lenye trela namba T 919 BVA
likiendeshwa na dereva asiyefahamika akitokea Morogoro kwenda Dodoma na
ambaye alikimbia baada ya ajali kutokea.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, dereva
huyo alijaribu kuyapita magari matatu mbele yake bila tahadhari na
kusababisha ajali hiyo.
Kaimu huyo alitaja majina ya waliokufa kuwa ni Francis Shija (70)
mkazi wa Nzega, mkoa wa Tabora, mwanamke mmoja anayekadiriwa kuwa na
umri wa miaka 45 hadi 50 ambaye hajatambulia jina , pamoja na mtoto
mdogo wa kiume ambaye bado hajatambuliwa kwa jina na umri wake ni kati
ya miaka mitatu hadi minne.
Aliwataja majeruhi waliolazwa katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa
Morogoro ni Kinazi Machum (38), ambaye ni Mhandisi na Mkazi wa Tabora,
Mathei Fidelis (30), mkazi wa Singida na Baraka Ruta (4) mkazi wa
Mwanza.
Wengine ni Juma Bilal (30) mkazi wa Nzega, Ebebeza Richard (22) mkazi
wa Mbeya, Hamis Mogela (30) mkazi wa Nzega, Pili Waziri (44) mkazi wa
Tabora na Prisca Shija (30) mkazi wa Nzega na wote wanaendelea vyema,
wakati maiti wakiwa wamehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha
Hospitali hiyo ya Rufaa.
Kaimu Kamanda alisema kuwa, polisi wanaendelea kumtafuta mtuhumiwa
ambaye ni dereva wa gari T 957 BUV aina ya Scania lenye trela namba T
919 BVA ili aweze kufikishwa katika vyombo vya sheria .