ZIARA ya Rais John Magufuli visiwani Pemba imemaliza ubishi wa
kisiasa na maneno ya kejeli kutoka kwa wafuasi wa Chama cha Wananchi
(Cuf) dhidi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) visiwani humu.
Wanachama hao walilazimika kuondoka katika uwanja wa Gombani ya kale
huku wakikata tamaa baada ya Rais kusema kwamba uchaguzi mwingine
utafanyika mwaka 2020 na kwamba Rais Ali Mohamed Shein ndiye kiongozi
mkuu wa halali wa Zanzibar aliyechaguliwa kikatiba.
Wafuasi wa CCM na Chama cha Wananchi kwa muda wa miezi saba sasa
wamekuwa katika malumbano ya kisiasa na mabishano ambapo wa Cuf wamekuwa
wakisema kuwa uchaguzi wa marudio wa Machi 20, mwaka huu ulikuwa
batili, jambo linalozifanya jumuiya za kimataifa zisiutambue.
Malumbano hayo yalishika kasi zaidi kutokana na ziara za mara kwa
mara za Katibu Mkuu wa Cuf, Seif Sharif Hamad nje ya nchi. Seif
aligombea urais Oktoba mwaka 2015 na kushindwa.
Ziara hizo zinatajwa kuwapa matumaini wana-Cuf kuwa serikali inayoongozwa na Dk Shein haitadumu.
Baadhi ya wakazi wa Pemba waliupongeza ujio wa Rais Magufuli wakisema
kuwa ujio wake umemaliza ubishi uliodumu kwa zaidi ya miezi saba kutoka
kwa wafuasi wa Cuf waliokuwa wakisisitiza kuwa Serikali iliyopo
madarakani itaondoshwa kwa nguvu za jumuiya za kimataifa.
Mkazi wa Chake Chake, Pemba, Asha Said, alisema amefurahishwa na
kauli za Rais Magufuli zenye ukweli na uwazi hasa alipowajibu wapinzani
kwamba hakuna uchaguzi mwingine hadi mwaka 2020.
Mabaraza ya Cuf katika jimbo la Chake Chake na Wawi, yalionekana
kudorora huku watu wengi zaidi wakiijadili hotuba ya Rais Magufuli
aliyoitoa Ijumaa visiwani Pemba.
Mfuasi mmoja wa Cuf katika eneo la Wawi, Pemba aliyejitambulisha wa
jina moja la Said, alisema wanamsubiri Katibu Mkuu wa chama chao, Maalim
Seif atoe kauli kuhusu hotuba hiyo ya Rais Magufuli.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mberwa Hamad Mberwa,
alisema hotuba ya Rais Magufuli ni mwiba mkali kwa wapinzani kwa kuwa
imeweka hadharani ukweli wa mambo.
Mberwa aliwataka wanachama na wafuasi wa CCM kusikiliza kauli za Rais
Magufuli za kuimarisha umoja na mshikamano kwa kujenga chama ili
kuendelea kuwepo madarakani. Alisema ukweli wameufahamu na kuujua na huu
si wakati tena wa kupoteza muda na kuingia katika malumbano ya kisiasa
kwa viongozi wanaoota ndoto za mchana.