Kwa ufupi
- Kesi ya kuhoji uhalali wake yafunguliwa
- Rafu Kamati za Bunge zatawala
Dar es Salaam/Dodoma. Bunge la Katiba linaloendelea mjini
Dodoma kwa sasa liko katika hatihati ya kuendelea baada ya kufunguliwa kesi ya
kuhoji madaraka yake.
Kesi hiyo ilifunguliwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam jana na Mwandishi
wa Habari Saidi Kubenea, kupitia kwa wakili wake Peter Kibatala, dhidi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Katika kesi hiyo iliyopewa usajili wa namba 28 ya mwaka 2014, Kubenea
anaiomba mahakama hiyo itoe tafsiri sahihi ya Mamlaka ya Bunge la Katiba.
Kubenea amefungua kesi hiyo akiomba mahakama itoe tafsiri hiyo, chini ya
vifungu vya 25 (1) na 25 (2) vya Sheria ya Marekebisho ya Katiba namba Namba 83
ya mwaka 2011.
Sambamba na kesi hiyo ya kuomba tafsiri ya mamlaka ya Bunge hilo, pia
Kubenea amewasilisha maombi mahakamani hapo akiiomba mahakama itoe zuio la muda
la kusimamisha Bunge hilo ili kusubiri uamuzi wa maombi ya tafsiri hiyo.
Maombi hayo ya kusimamisha Bunge hilo kwa muda yaliyopewa usajili wa namba
29 ya mwaka 2014, pamoja na maombi ya msingi ya tafsiri ya mamlaka ya Bunge
yote yalifunguliwa mahakamani hapo jana chini ya Hati ya Dharura.
Katika kesi hiyo ya msingi anaiomba Mahakama hiyo itoe tafsiri sahihi ya
masharti ya vifungu hivyo vya sheria hiyo na pia itamke kama Bunge hilo lina
mamlaka ya kubadilisha maudhui ya Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba na kwa kiwango gani.
Kwa mujibu wa hati ya madai, Kubenea anadai kuwa msingi wa kesi hiyo
unatokana na uamuzi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Desemba
Mosi, 2011, lililopitisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Anasema sheria
hiyo ilikuwa na lengo la kuratibu mchakato wa kutungwa kwa Katiba Mpya ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Anaendelea kusema kuwa kutokana na sheria hiyo, Rais aliunda Tume ya
Mabadiliko ya Katiba pamoja na mambo mengine vilevile kukusanya maoni ya
wananchi kuhusu mapendekezo ya Katiba Mpya na kwamba kwa msingi huo Tume hiyo
iliandaa Rasimu ya Katiba.
Anadai kuwa baada ya Tume hiyo kuundwa iliendelea kukusanya maoni ya
wananchi yaliyotolewa katika mikutano ya hadhara na katika miundo tofauti ikiwamo
mabaraza ya Katiba yaliyoanzishwa kila wilaya kwa lengo hilo.
Hati hiyo inaendelea kueleza kuwa kwa mujibu wa takwimu halisi za tume
hiyo, jumla ya watu 333,537 walitoa maoni yao katika nyanja tofauti,
tofauti za mapendekezo ya Katiba, ambayo ndiyo Tume ya Mabadiliko ya Katiba
iliyatumia kuandaa Rasimu ya Katiba Mpya.
Inaendelea kueleza hati hiyo kuwa baada ya Rais kukabidhiwa rasimu ya mwisho
Desemba 8, 2013, kwa mujibu wa vifungu vingine vya sheria hiyo, aliunda Bunge
la Katiba kwa lengo la kujadili Rasimu ya Katiba na hatimaye kupata Katiba
Mpya.
Hata hivyo, kwa mujibu wa hati hiyo baada ya Bunge la Katiba kuundwa,
mjadala uliibuka ndani na nje ya misingi ya kisheria kuhusu mamlaka
yake, kama Bunge linaweza kwenda kinyume na Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na
tume hiyo.