Wizara ya Maji imelipuliwa Bungeni kwa kutoa takwimu za uongo katika utekelezaji wa miradi ya maji nchini ambayo imesababisha wananchi kukosa huduma hiyo muhimu huku baadhi ikiwa haijakamilika kwa wakati unaotakiwa na mingine kutotekelezwa kabisa.
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Aidha, Wabunge wamehoji
wakandarasi wanaopewa tenda za miradi ya maji bila kuwa na vigezo na
kusababisha pesa nyingi kupotea na miradi kukwama.
Wakichangia Bajeti ya Wizara ya Maji
jana, Baadhi ya Wabunge hao ni Mbunge wa Rungwe (CCM), Prof. David Mwakyusa,
Esther Bulaya (Viti Maalum – CCM), Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy
(CCM), Mbunge wa Mbozi Mashariki, David Silinde (Chadema) na Ezekeil Wenje
(Nyamagana), waliilalamikia wizara hiyo kwa kutoa takwimu za uongo na kuweka
makandarasi wasio na vigezo.
Hoja hiyo, ilimfanya Mbunge Wenje,
kuomba mwongozo wa Spika wa Bunge, Anne Makinda, wa kumtaka waziri atolewe nje
ya bunge ili akakae na watalaam wake na kuleta takwimu sahihi bungeni
zitakazojadiliwa.
Hata hivyo, Spika wa Bunge,
alimtaka Mbunge kuketi na kumtaka ukifika wakati wake achangie hoja yake.
Katika hoja hiyo, Wenje alisema
wabunge wakati wakichangia bajeti hiyo wamelalamikia takwimu zilizotolewa na
waziri kuwa si za kweli na kutoa mifano kadhaa ya idadi ya vijiji vinavyopatiwa
huduma hiyo kuwa ndogo kuliko iliyotajwa.
Alitoa mfano wa Mbunge Azza
aliyesema vijiji 53 vilivyotajwa kwenye takwimu zlizotolewa na waziri kuwa
vinapata huduma ya maji kwenye wilaya yake ni vinane tu vinavyopata huduma
hiyo.
“Tusingekuwa bunge la kufanya rubber
stamp (muhuri), waziri alitakiwa afukuzwe ndani ya bunge akakae na watalaam
wake na atuletee taarifa sahihi ili tuje tuijadili,” alisema.
Alisema vituo hivyo hewa
vinavyotajwa kutoa huduma za maji vimetumia pesa ya walipa kodi na kuhoji
hizo pesa zinakwenda wapi.
Wenje aliongeza kuwa miradi mingi ya
maji imejaa rushwa huku watu wakitumia pesa hizo kujinufaisha kwa kujenga
nyumba na kununua magari ya thamani.
Alisema sakata hilo la miradi hewa
ya maji halina tofauti na chenji ya rada na kuongeza ni ufisadi mtupu
unafanyika katika miradi hiyo.
Kwa upande wake Prof.
Mwakyusa, alisema maji ni huduma muhimu kwa jamii na waziri anaposema
watu wanaopata maji vijijini kwa sasa ni asilimia 50-55, aeleze ni vijiji vipi
na vingapi vinapata huduma hiyo.
Alisema matumizi ya takwimu ni
lazima yatumike vizuri badala ya kupotosha wananachi na kwamba kuna baadhi ya
vijiji ambavyo mpaka sasa havina maji na kuitaka wizara hiyo ionyeshe
mtawanyiko wa vijiji ambavyo vinapata huduma hiyo.
Prof. Mwakyusa pia aliitaja miradi
ya Kidunda, Kimbiji, Mpera na Masoko ambayo ni ya siku nyingi itengenewe bajeti
ili iweze kutekelezeka.
Mbunge wa Rungwe (CCM), Prof. David Mwakyusa
Akiunga mkono hoja hiyo Bulaya,
alisema kuna wakandarasi wanaolipwa pesa bila kukamilisha miradi ya maji na
kutoa mfano wa Mradi wa Mgeta Nyangaranga, ambapo amepewa pesa Sh. Milioni 450
lakini mpaka sasa hajakamilisha mradi huo.
Alitaja mradi mwingine kuwa ni wa
Bunda ambao ni wa muda mrefu na wananchi wanahangaika kwa miaka tisa
kupata huduma hiyo. Aidha, mkandarasi aliyewekwa hatimizi wajibu wake na wakati
mwingine wizara inampa mabomba huku akiwa ameshalipwa pesa wakati huko Rorya
walimkataa.
“Ni vigezo gani mnavyotumia
kuwapa miradi hawa wakandarasi kwa sababu wakandarasi wengi wanaopewa pesa
hawakamilishi miradi na hawana vigezo,” alisema.
Chanzo Nipashe