MSHAMBULIAJI wa Yanga, Juma Mahadhi, amesema kuwa yuko radhi kuachwa na kikosi cha mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara badala ya kupelekwa kwa mkopo katika klabu nyingine
 Mahadhi alitua Yanga msimu uliopita akitokea Coastal Union ya jijini Tanga na katika mechi dhidi ya Kombe la Shirikisho dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), straika huyo alionyesha kiwango cha juu.
Taarifa kutoka katika klabu hiyo zinaeleza kuwa Yanga wana mpango wa kumpeleka Mahadhi kwa mkopo katika klabu ya Singida United ambayo sasa inanolewa na Mholanzi Hans van der Pluijm.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mahadhi alisema kuwa tayari ameshapata ofa kutoka katika klabu za ndani na nje ya nchi lakini anaheshimu mkataba wake wa mwaka mmoja uliobakia ndani ya Yanga.
"Siko tayari kutolewa kwa mkopo, nina ofa za ndani na nje ya nchi lakini nasubiri kujua hatima yangu ndani ya Yanga, ni bora waniache nikatafute riziki mahali kwingine nitakaporidhia mwenyewe, naamini nitakifanya kile nilichokionyesha katika mechi ya Mazembe, uwezo bado ninao," alisema Mahadhi.
Mshambuliaji huyo aliongeza kuwa anaamini atakapokutana na viongozi wake watazungumza na kufikia muafaka kuhusiana na suala hilo kwa kuzingatia maslahi ya pande zote mbili.


    TANGAZO 
 
Top