Fumbo kuhusiana na mtu mwenye sifa za kuwa Waziri Mkuu wa serikali ya awamu ya tano ya Rais Dk. John Magufuli limeanza kufumbuliwa.
Hali
hiyo inatokana na kile alichokidhihirisha Magufuli siku moja baada ya kuapishwa
kwake na pia baada ya hapo wakati alipochukua maamuzi kadhaa ya vitendo,
ikiwamo kutoa maelekezo muhimu yaliyodhihirisha aina ya Waziri Mkuu
atakayemteua.Kwa mujibu wa muundo wa serikali, Waziri Mkuu ndiye kiongozi wa
shughuli za serikali bungeni, ambaye mbali ya kuwa kinara wa mawaziri wengine,
ndiye anayetakiwa pia kutoa maamuzi mazito linapojitokeza jambo linalomlazimu
kufanya hivyo.
Wakizungumza
na Nipashe, baadhi ya wafuatiliaji wa masuala ya siasa na uongozi nchini
wamesema hatua alizochukua Magufuli kuanzia siku ya kwanza ya kuapishwa kwake
zinatoa picha ya wazi aina ya watu atakaotaka kuwa nao katika serikali yake.
Baada
ya kuapishwa Novemba 5, 2015, kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, Dk.
Magufuli alianza kazi siku hiyo hiyo kwa kutoa hotuba iliyosisitiza juu ya
kauli mbiu yake ya ‘hapa kazi tu’ katika kutumikia wananchi, kuwafariji
waliokuwa wapinzani wake katika urais huku akiwasihi waungane naye kuijenga
Tanzania imara na pia alimteua Mwanasheria Mkuu, George Masaju, huku pia
akitangaza siku ya kuanza Bunge kuwa ni Novemba 17.
“Ratiba
yake katika siku ya kwanza aliyoapishwa ilikuwa ngumu kutokana na wageni wengi
waliomtembelea lakini bado hakutaka kuchelewa katika kuteua Mwanasheria Mkuu.
Na siku iliyofuata (Ijumaa) akaonyesha yeye ni Rais wa aina gani kwa kufanya
ziara ya ghafla kwenye Wizara ya Fedha na kujionea aina ya watendaji waliopo.
Yote haya yanatosha kufichua sifa za mawaziri atakaowateua,” alisema John
Jacob, mkazi wa Magomeni jijini Dar es Salaam ambaye ni mmoja wa wafuatiliaji
wa siasa.
“Hivi
sasa siyo kazi tena kubashiri aina ya Waziri Mkuu tutakayekuwa naye. Magufuli
ameonyesha wazi kwamba yeye ni mchapakazi na hivyo hawezi kukubali wababaishaji
au kuchagua mtu kwa sababu yoyote isiyohusiana na kazi,” alisema Latifa
Abdallah, mfuatiliaji pia wa masuala ya siasa mwenye maskani yake jijini
Arusha.
DALILI
YA SIFA MUHIMU ZA WAZIRI MKUU MPYA
Baada
ya uteuzi wa Mwanasheria Mkuu alioufanya siku ya kuapishwa kwake (Alhamisi),
Magufuli alisubiri saa chache tu kabla ya kutembea kwa miguu kutoka ofisini
kwake hadi katika jingo la Wizara ya Fedha ambako alifanya ziara ya kustukiza,
akiingia kila ofisi kuona shughuli za ujenzi wa taifa zinavyoendelea.
Huko,
baada ya kukuta watendaji wake wakiwa hawapo ofisini huku akipewa majibu kuwa
wameenda kunywa chai, Magufuli alikuja juu na kutoa maagizo muhimu juu ya dhana
ya kuchapa kazi.
Ni
wazi kwamba kwa kufanya hivyo, Magufuli anaonyesha kuwa Waziri Mkuu wake
atapaswa kuwa mtu wa vitendo zaidi na siyo maneno mengi.
Kadhalika,
utoaji wa maamuzi kuanzia siku ya kwanza ni sifa muhimu ya kile alichokuwa
akikisisitiza wakati wa kampeni kuwa kamwe, hatavumilia mawaziri wanaopenda
majibu ya ‘tuko mbioni’, ‘tuko kwenye mchakato’, ‘tuko kwenye hatua nzuri’ wala
‘tuko kwenye hatua za mwisho’. Ni kazi tu.
Aidha,
Magufuli ameonyesha vilevile kuwa Waziri Mkuu wake atakuwa ni mtu wa kutoa
maamuzi kwa kasi. Sifa hii inatokana na muda alioutumia katika kutangaza jina
la Mwanasheria Mkuu na pia siku ya kuanza kwa Bunge la 11.
Tofauti
na ilivyozoeleka, juzi Jumamosi haikuwa siku iliyopita burebure kwa Magufuli.
Alifanya kikao kizito na makatibu wakuu, naibu makatibu wakuu, gavana wa Benki
Kuu (BoT) na Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Katika kikao
hicho, Magufuli alitoa maelekezo kadhaa yaliyofichua sifa nyingine muhimu
atakazokuwa nazo Waziri Mkuu wake na pia mawaziri wengine.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ikulu kuhusiana na kile kilichoijiri kwenye
kikao hicho, ni kwamba Rais Magufuli aliagiza kufutwa mara moja kwa safari za
nje za mawaziri na viongozi wengine wa juu serikalini na kwenye taasisi za
umma.
Aliagiza
kuwa masuala yote ya nje ya nchi yatekelezwe na mabalozi waliopo huko na
kwamba, kukiwa na ulazima, basi safari hizo ni lazima ziidhinishwe na yeye
(Rais) au Katibu Mkuu Kiongozi, Ikulu. Rais Magufuli aliagiza kuwa anachotaka
ni kuona viongozi wakifanya ziara nyingi kwa wananchi vijijini na kuwatatulia
kero zao.
Hii
ni dalili nyingine ya wazi kuwa Waziri Mkuu ajaye hatakuwa mtu wa kusafiri nje
mara kwa mara na badala yake, atakuwa ni mtu wa kuwa karibu na wananchi huku
akisimamia shughuli za serikali kwa umakini zaidi.
Agizo
jingine muhimu alilotoa Magufuli ni kutaka kuona viongozi hao wakiweka mikakati
mbalimbali itakayoanza kutekelezwa mara moja ifikapo Januari 2016, na mojawapo
ya mikakati hiyo iwe ni ahadi yake ya kutoa elimu bure kuanzia shule ya msingi
hadi kidato cha nne.
Aliagiza
pia kuwapo kwa mikakati ya kuhakikisha kuwa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya
juu inatolewa bila shida.
Hii
maana yake ni kuwa sifa mojawapo ya Waziri Mkuu itakuwa ni kuwa mzuri katika
kuandaa mikakati na kusimamia utekelezaji kwa umakini ili kuleta matokeo
chanya, tena kwa wakati.
Kadhalika,
katika kikao hicho, Dk. Magufuli alisisitiza kuwa ni lazima kila mtendaji wa
serikali kuzingatia, kufuata sheria na taratibu ili taifa lisonge mbele
kimaendeleo na kwa ufanisi zaidi. Hii ni dalili kuwa Waziri Mkuu wake na pia
mawaziri wengine ni lazima wawe waumini wazuri wa sheria na taratibu, na siyo
watu wa kufanya kazi kwa mazoea.
Rais
Magufuli alimuagiza Kamishna wa TRA kusimamia kwa umakini ukusanyaji wa mapato
nchini na kuhakikisha kuwa kero ndogo ndogo kwa wananchi zinatatuliwa kama
alivyoahidi.
Aliitaka
TRA kuhakikisha inakusanya mapato hayo kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa zaidi
na wale wanaokwepa kodi bila kuogopa mtu wala taasisi yoyote.
Hii
ni ishara kuwa sifa nyingine muhimu kwa Waziri Mkuu wa Magufuli ni kufanya kazi
kwa kujiamini, lengo likiwa ni kuongeza mapato ya serikali na katika kutekeleza
hili, anatakiwa kujiamini muda wote kwani Rais atakuwa akimuunga mkono katika
kila hatua na hakuna atakayefanya ujanja ujanja kwa kutumia jina la ‘Rais
Magufuli’.
Alisisitiza
vilevile kuwa katika serikali yake, mtu wa kutoa maamuzi vinginevyo zaidi ya
hayo aliyowapa ni yeye (Rais), au Makamu wa Rais.
Umakini
katika kuhakikisha kuwa serikali haipati hasara kutokana na manunuzi
yasiyozingatia sheria, au yenye harufu ya rushwa, ni eneo jingine atakalopaswa
kuwa nalo Waziri Mkuu mpya wa serikali ya awamu ya tano.
Katika
kikao hicho, Magufuli alisema suala la manunuzi limekuwa likitumika vibaya na
kuwa mwanya wa kuiibia serikali kwa watu kuongeza bei ya vitu hata kama ni vya
bei ndogo katika jamii.
“Ikitokea
suala hilo likagundulika kwa watu kuongeza bei ya vitu, watendaji
watawajibishwa mara moja,”alisema.
Katika
hili, ipo sifa nyingine anayotarajiwa kuwa nayo Waziri Mkuu mpya, ambayo ni
kuwa na jicho la ziada kuhakikisha kuwa serikali haipati hasara kwa kuuziwa
vitu kwa bei ya juu kuliko iliyopo sokoni.
UHODARI
BUNGENI
Sifa
nyingine muhimu kwa Waziri Mkuu ni kuwa mzoefu wa kukabili changamoto za hoja
moto za wapinzani bunegni kwani katika Bunge lijalo, kambi ya upinzani itakuwa
na wabunge 121. Kwa sababu hiyo, ni wazi kwamba mtu atakayeteuliwa na Rais
Magufuli kwa nafasi ya Waziri Mkuu ni lazima atakuwa na sifa ya kukabiliana na
maswali ya wabunge machachari wa upinzani pale inapobidi, ikiwamo wakati wa
maswali ya papo kwa papo.
Kwa
ujumla, kama ilivyowahi kuripotiwa katika gazeti hili wiki iliyopita, sifa
muhimu za ujumla kwa Waziri Mkuu wa Magufuli zatarajiwa kuwa uadilifu, kwa
maana ni lazima awe mtu asiyekuwa na chembe ya kashfa, hasa zinazohusiana na
rushwa kama ilivyo kwa mwenyewe (Rais Magufuli); Kujiamini kiasi cha kutoa
maamuzi magumu na kwa wakati kwa ajili ya maslahi ya taifa; kufanya kazi kwa
pamoja na siyo kusaka umaarufu binafsi kiasi cha kumpiku Rais; Uwezo wa
kusimamia utekelezaji wa mipango ya serikali; Kukubalika ndani na nje ya Chama
Cha Mapinduzi (CCM).
CHANZO NIPASHE