Aliyekuwa mgombea Urais wa jamhuri wa Muungano wa Tanzania wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kupitia Umoja wa Katiba ya wananchi (Ukawa)
CHANZO: NIPASHE
Edward Lowassa, amehoji
maswali matatu kwa Rais Dk. John Magufuli.Katika taarifa yake kwa vyombo vya
habari jijini Dar es Salaam jana, Lowassa amemtaka Rais Magufuli baada ya
kusema hakuna mtoto atakayelipa ada kuanzia Januari, mwakani, atamke mustakabali
wa wanafunzi walioko shuleni kama wataguswa na hatua hiyo au la.
Lowassa amesema kwa upande
wake ahadi ya elimu bure aliyokuwa akiinadi wakati wa kampeni, ilikuwa ni
kuanzia shule ya awali hadi chuo kikuu na kwamba hata wale walioko mashuleni,
wangeguswa na hatua hiyo.
“Niliahidi watoto wote walioko
na watakaoanza shule kuanzia kindergarten (shule ya awali) hadi chuo kikuu,
serikali yetu ingegharimia. Na nilitangaza kufuta michango yote shuleni ili
kumpunguzia mzigo mwananchi,” alisisitiza Lowassa ambaye amekataa kuyatambua
matokeo ya ushindi wa Dk. Magufuli akidai kuwa yeye ndiye aliyeshinda kwa
asilimia 62 ya kura zote zilizopigwa.
Kuhusu suala la mikopo kwa
wanafunzi wa elimu ya juu, Lowassa amesema yeye alishaweka wazi kuwa elimu
ingekuwa bure hadi chuo kikuu.
“Vijana hawa wanahangaika na
mikopo na nasikia ni asilimia 17 tu kati ya wanafunzi 70,000 ndiyo waliopata
mikopo. Sera ya Chadema na Ukawa kwa ujumla, ni kufuta kabisa shida hizi kwa
serikali kufadhili elimu yao,” alifafanua Lowassa katika taarifa yake hiyo. Kwa
msingi huo, Ukawa kupitia kwa aliyekuwa mgombea wao wa urais, Lowassa,
umewataka wananchi kutofautisha ahadi ya elimu bure iliyotolewa na Rais
Magufuli na ile iliyotolewa na Ukawa.
Lowassa alisema Magufuli
ametoa maelekezo kwa watendaji wa serikali kuweka mikakati ya kutekeleza ahadi
yake kuanzia Januari, mwakani kwamba hakuna mtoto atakayelipa ada.
Hata hivyo, amesema hajaeleza
waziwazi hatma ya wanafunzi walioko mashuleni kama wataguswa na hatua hiyo au
la.