Chama cha demokrasia na maendelea (Chadema) kimeweka mkakati utakaowafanya makada wake wavamie majimbo yanayoshikiliwa mapema na CCM, huku wakichelea kuingia kwenye majimbo yaliyo chini ya chama hicho kikuu cha upinzani.
Mkakati huo ulitangazwa jana na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe wakati
akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Mongella mjini hapa,
mkutano ambao ulifurika maelfu ya watu.
Mbowe alitangaza kupiga marufuku wanachama wa Chadema kuanza kutangaza nia
kwenye majimbo ambayo wenzao wanayashikilia hadi hapo Bunge la Jamhuri ya
Muungano litakapovunjwa.
Lakini alisema wanachama wa Chadema wanaruhusiwa kuanza purukushani kwenye
majimbo ambayo yanashikilia na vyama vingine hasa chama tawala cha CCM ambacho
kinashikilia majimbo mengi.
“Naomba ifahamike Chadema ni zaidi ya ubunge, tunahitaji amani na siyo
kuharibu chama. Chadema itasimamisha watu makini kwenye maeneo yote katika
uchaguzi huu,” alisema mwenyekiti huyo ambaye yuko kwenye ziara ya mikoa ya
Kanda ya Ziwa.
Mbowe ambaye hakugusia suala la Ukawa katika mkutano huo, alisema kuwa
utaratibu utaandaliwa wa kupata wagombea na kwamba hata waliokuwa wabunge,
wasijihakikishie kuwa watapitishwa tena kwenye maeneo yao wanayoyaongoza sasa.
“Tutakuja na utaratibu mwingine. Hata wabunge wa Chadema waliokuwa katika
maeneo hayo, wasidhani kwamba watabakia hapo. Tutasimamisha mtu anayekubalika
na watu wote, na utaratibu ukiwekwa, hata aliyekuwa mbunge anaweza kuondolewa,”
alisema Mbowe.
Alisema kuwa Chadema inaamini kuwa katika kila eneo kuna mtu wake ambaye ni
makini na ni wazi atashinda.
Vyama vinne vya upinzani, Chadema, NLD, NCCR-Mageuzi na CUF vimekubaliana
kusimamisha mgombea mmoja kuanzia kwenye uchaguzi wa madiwani hadi rais. Vyama
hivyo, vilivyo chini ya mwavuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),
vimekubaliana kuwa kila chama kipate mgombea wake na baadaye vitachambua
anayekubalika na wengi.
Ainanga Nec
Akizungumzia mwenendo wa uboreshaji wa Daftari la Wapigakura, Mbowe alisema
Taifa kwa sasa liko kwenye giza nene kutokana na maandalizi mabovu ya Tume ya
Taifa ya Uchaguzi(Nec).
Mbowe alisema kucheleweshwa kwa kazi ya uandikishaji wapigakura ni sehemu ya
njama za CCM kupitia Serikali yake inayotamani kutumia nafasi hiyo ili
kuendelea na hujuma katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Mbowe, ambaye aligombea urais mwaka 2005, alisema Nec inachelewesha kazi
hiyo ili kuibeba CCM katika uchaguzi mkuu kwani kukamilika kwa daftari hilo
kunaonekana kunaitia hofu CCM.
“Kuna wananchi wengi, zaidi ya milioni 26 wanatakiwa kuandikishwa na muda
uliobakia ni mfupi. Walichelewesha kwa makusudi ili kuisaidia CCM iendelee
kututawala kwa nguvu ya watu wachache watakaokuwa na sifa za kupiga kura, “
alisema.
“Kwa njama hizo, tunamuomba Rais (Jakaya) Kikwete amalizie muda wake kwa
amani na asituharibie amani ya nchi yetu kwa kutengeneza hujuma. Bora amalize
muda wake ili akapumzike kijijini kwao.”
Mbowe alisema mpaka sasa Rais Kikwete ndiye wa kulaumiwa kwa maandalizi hayo
ya Uchaguzi Mkuu kutokana na dalili zinazoonekana kwa sasa.
“Kampeni ni siku 72 kabla ya Uchaguzi Mkuu na mpaka sasa ni miezi mitatu tu
imebakia kabla ya kuanza kampeni, lakini hakuna dalili za maandalizi yoyote.
Haya yote yamechangiwa na Serikali yenye maandalizi mabovu,” alisema Mbowe.
Mbowe pia alishangazwa na kitendo cha Serikali kutumia fedha nyingi katika
mchakato wa Katiba bila mafanikio yoyote yale, lakini hakuna kiongozi
aliyewajibishwa kwa hasara hiyo.
Katika hatua nyingine, Mbowe alifafanua kuhusu urais nafasi ya urais kupitia
Ukawa akisema, kwa sasa lengo lao kwa pamoja siyo bora kupata urais, bali ni
kuangalia kiongozi gani atakayesimama kuwakilisha Ukawa katika nafasi hiyo.
“Kwa hivyo CCM na watu wengine wasidhani kwamba Ukawa tutagombana kwa sababu
hiyo, tumejipanga na dhamira yetu ndiyo nguvu ya Watanzania walioridhia
kuungana kwetu. Tunaamini CCM lazima ing’oke katika uchaguzi huu,” alisema
Mbowe.
Katika hatua nyingine, Mbowe pia aliwaonya baadhi ya wanasiasa wanaounda
Ukawa, kuanza kutangaza nia kwenye majimbo yenye wabunge kwa sasa. Alisema nafasi
hiyo ya kutangaza nia itapatikana baada ya Bunge kuvunjwa.
Mafunzo ya FP200
Akizungumzia mkakati wa kutoa mafunzo kwa vijana wa chama hicho FP200, Mbowe
alisema kuwa hata kama IGP ataweka pingamizi, lazima watatekeleza azimio hilo.
Alisema IGP, akitaka kuwakachukulia hatua basi, yeye atakuwa muhusika namba
moja.
“Hata Jeshi la Polisi wakizuiua lazima mafunzo yatafanyika na kama wanataka
kuchukua hatua basi Mbowe akamatwe,” alisema Mbowe.
Choanzo Mwananchi